Na Mwandishi Wetu, Shinyanga

Watu 25 wanahofiwa kufukiwa kwenye mashimo waliyokuwa wakichimba dhahabu kwenye mgodi wa Nyandolwa katika Kijiji cha Mwongozo Kata ya Mwenge Halmashauri ya Wilaya Shinyanga.

Mmiliki wa mgodi huo, Fikiri Mnwagi alisema hayo wakati akitoa taarifa kwa kamati ya ulinzi wa usalama ya mkoa na wilaya. Amesema mashimo hayo matatu yalikuwa katika ukarabati.

Amesema jana asubuhi lilitokea tetemeko na kusababisha ardhi ya eneo hilo kutitia na kufunika watu 25 ambao ni wafanyakazi na mafundi waliokuwa wakifanya ukarabati.

“Tumeanza uokozi na mawasiliano yaliyokuwa yakifanyika kati ya watu sita wa duara namba 106 yameleta matunda na watu watatu wameokolewa leo Agosti 12, 2025 zoezi la uokoaji bado linaendelea,” amesema.

Mnwagi amesema hawakufanikiwa kuwasiliana na waliofukiwa kwenye mashimo namba 20 na 103 na walikuwa wakiendelea na juhudi za uokozi ikiwa ni pamoja na kuchimba shimo la ziada ili kuwafikia sanjari na kupitisha maji na chakula.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro akiwa kwenye eneo la uokozi amesema baada ya kufika eneo la tukio aliomba wananchi wawe watulivu wakati kazi ya uokozi ikiendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita akizungumza na wananchi na wafanyakazi wa eneo hilo, alitoa salamu za pole na kushukuru kazi waliyoanza kuifanya ya uokozi.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Joseph Shahibu alidai kuna vijana wanaoweza kusaidia kazi ya uokozi hivyo aliomba waruhusiwe washiriki.