Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Watu 259 wamepata huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo inayotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi ya Umma yanayofanyika kwenye Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa jana jijini Dodoma na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha Maucky wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma hiyo ya upimaji na matibabu ya moyo.

Dkt. Maucky alisema wagonjwa waliowaona  tangu kuanza kwa maonesho hayo wengi wao ni wanaume ukilinganisha wa wanawake hali hiyo imekuwa ni tofauti na maeneo mengine ambayo wanakwenda kutoa huduma kama hiyo ambako idadi ya wanawake wanakuwa ni wengi zaidi.

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Upendo Mwaipopo akimpima shinikizo la damu mkazi wa Dodoma aliyefika katika banda la taasisi hiyo jana kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

“Kati ya watu 259 tuliowapa huduma wanaume walikuwa 168 na wanaweka 91 mwitikio umekuwa ni mkubwa zaidi kwa wanaume ukilinganisha na wanawake na watu tuliowaona wengi wao walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, kisukari, moyo kutanuka na shida ya valvu kutokufanya kazi vizuri”, alisema Dkt. Maucky.

Dkt. Maucky alisema mgonjwa aliyekutwa na shida ya valvu ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufanyiwa vipimo vya moyo na hakuwa anajijua kuwa na shida, baada ya vipimo valvu yake ilikutwa na shida na hivyo kupewa rufaa ya kwenda JKCI kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kuibadilisha.

Afisa Muuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hania Bwahama akitoa elimu ya jinsi moyo unavyofanya kazi kwa mwananchi aliyefika katika banda la taasisi hiyo jana kwa ajili ya kupata elimu ya magonjwa ya moyo na kufahamu huduma zinazotolewa na JKCI wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma

“Ninawaomba wananchi mtumie nafasi hii kujitokeza kwa wingi kupima afya za mioyo yenu huduma hii inatolewa bila malipo yoyote yake, tumieni siku tatu zilizobaki katika maonesho haya kuja kupima na kupata ushauri wa jinsi ya kuepukana na magonjwa haya”, alisisitiza Dkt. Maucky.

Kwa upande wa wananchi waliopata huduma ya ushauri, upimaji na matibabu ya moyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kufahamu afya za mioyo yao.

“Mimi ni mkazi wa Kigamboni Dar es Salaam nilifika hapa kupata huduma katika Wizara ya Ardhi, baada ya kusikia kuna huduma za upimaji wa moyo nimekuja kupima nimepata huduma nzuri na ninashukuru baada ya vipimo moyo wangu uko vizuri”.

“Daktari amenishauri niendelee kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora, ninawaomba wananchi wenzangu mjali afya zenu kwanza kabla ya vitu vingine kwa kuja kupima kwani huduma za upimaji zinatolewa bure hulipii chochote kile”, alisema Elisafi Kifimbo.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha akimuhudumia mwananchi aliyefika katika banda la taasisi hiyo jana kwa ajili ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya moyo  wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

“Baada ya kufika hapa na kufanyiwa vipimo nimekutwa na tatizo la uzito mkubwa, mtaalamu wa lishe  amenishauri kufanya mazoezi na amenielekeza aina ya vyakula vya kula ili nipunguze uzito”.

“Nashukuru huduma niliyopata ni nzuri na sijalipia kitu chochote, ninaiomba serikali itusaidie kutoa huduma hizi mara kwa mara ili sisi ambao uwezo wetu kiuchumi  ni mdogo tuweze kupata huduma za kibingwa za matibabu ya moyo ambazo zitatupunguzia gharama ya kulipia na kuzifuata Dar es Salaam”, alishukuru Ester Masingija mkazi wa Ihumwa