Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Same
Watu zaidi ya 34 wamepoteza maisha na wengine 16 kujeruhiwa baada ya kutokea ajali ya barabarani leo asubuhi, Jumamosi Juni 28, 2025, katika eneo la Sabasaba, Kata ya Same, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.
Ajali hiyo imehusisha basi kubwa la Kampuni ya Channel One lililokuwa likitokea Moshi kuelekea Tanga na basi dogo aina ya Coaster lililokuwa likitoka wilayani Same kwenda Moshi. Magari yote mawili yamewaka moto mara baada ya kugongana uso kwa uso, hali iliyosababisha taharuki na vifo vinavyohofiwa kuwa vingi.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi, amethibitisha ajali hiyo na kueleza kuwa juhudi za uokoaji zimefanikisha kuokoa watu 16 hadi sasa.

“Watu zaidi ya 16 wameokolewa katika ajali hii iliyohusisha basi kubwa na dogo, ambayo yaliwaka moto. Tunashukuru kwa ushirikiano wa haraka kutoka kwa wananchi na vyombo vya uokoaji.
“Tupo njiani kuelekea eneo la tukio, lakini taarifa za awali ni kwamba basi la Kampuni ya Channel One lililokuwa likitokea Moshi kuelekea mkoani Tanga na Coaster iliyokuwa inatoka Same kuja Moshi Mjini yamegongana na kuwaka moto.” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa mamlaka zipo kazini kuhakikisha kila mtu anapokea msaada unaohitajika haraka iwezekanavyo.
“Tunaendelea na juhudi za uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na wananchi wa maeneo ya jirani. Lengo ni kuhakikisha wote waliokumbwa na mkasa huu wanapatiwa msaada wa haraka,” amesema Kasilda.

Hadi sasa idadi kamili ya watu waliopoteza maisha haijajulikana, huku kazi ya kuzima moto, kutoa miili na kuokoa manusura ikiendelea. Wahanga waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu katika vituo vya afya vilivyo karibu na eneo la tukio.
Wananchi wametakiwa kuwa watulivu na kuepuka kukaribia eneo la tukio ili kurahisisha kazi ya uokoaji, huku uchunguzi wa chanzo cha ajali ukiendelea .

