Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewatia mbaroni watu 46 kwa tuhuma za kujihusisha na makosa mbalimbali ya kijinai ikiwemo unyang’anyi wa kutumia nguvu, uvunjaji wa nyumba na maghala (godown) pamoja na wizi wa mali tofauti.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 24, 2026, ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro, amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni zilizofanyika kuanzia Januari 30 hadi Februari 24, 2026.
Kamanda Muliro ameeleza kuwa baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakitumia pikipiki na silaha za jadi kama mapanga kutekeleza uhalifu huo, hasa katika maeneo ya pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam.
Amesema pia baadhi yao walijihusisha na kuvunja nyumba mchana na usiku na kuiba vifaa mbalimbali, huku wengine wakijihusisha na kununua na kuuza mali za wizi.
Katika operesheni hizo, Jeshi la Polisi limekamata pikipiki zaidi ya 20 (maarufu kama vishandu), simu 110, runinga, redio na vifaa vingine vya kielektroniki. Pia zimekamatwa funguo maalum zenye uwezo wa kufungua aina mbalimbali za kufuli pamoja na gari aina ya Toyota Noah yenye namba ya usajili T.457 CQF iliyokuwa ikitumika kusafirisha mali za wizi.
Kamanda Muliro amewataja baadhi ya watuhumiwa kuwa ni Rashidi Mtunguja maarufu “Msamba” na wenzake wanne waliokamatwa eneo la Jangwani; Issa Nasoro Kurukutu na wenzake wawili waliokamatwa Gongolamboto; pamoja na Nicholas Abdallah Said mkazi wa Manzese.
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo amesema Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji wa kuwakamata wahusika wote wa vitendo vya kihalifu, kabla au baada ya kutekeleza uhalifu, kwa kuzingatia misingi ya kisheria ikiwemo kukusanya ushahidi, kuwafikisha watuhumiwa Ofisi ya Mashtaka na hatimaye mahakamani.
Ameongeza kuwa baadhi ya watuhumiwa tayari wamehukumiwa vifungo vikali, ikiwemo kifungo cha maisha jela kwa makosa ya ubakaji wa kundi na unyang’anyi wa kutumia silaha.
“Miongoni mwa waliohukumiwa ni Mwita Marwa na wenzake wawili waliopatikana na hatia katika Mahakama ya Kigamboni, Adam Samiro aliyehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela, pamoja na Jafari wa Chang’ombe na Omari Omari wa Mbande waliopata adhabu kali katika Mahakama ya Temeke,” amesema Muliro.
Akizungumzia usalama barabarani, SACP Muliro amesema Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua dhidi ya madereva wanaokiuka sheria, hususan wanaotumia barabara za mwendokasi.
Amesema jumla ya madereva 250 walikamatwa katika kipindi hicho, wakiwemo waendesha bodaboda 167, bajaji 19 na magari 64, hatua iliyolenga kupunguza ajali na kero kwa watumiaji wa barabara.
Jeshi la Polisi limewasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na kuahidi kuendelea kulinda usalama ili shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa ziendelee kufanyika kwa amani.




