Utapiamlo umesababisha vifo vya watu 63 katika muda wa wiki moja pekee, wengi wao wakiwa wanawake na watoto katika mji uliozingirwa wa El-Fasher nchini Sudan ambako hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya.
Taarifa hiyo imetolewa Jumapili (11.08.2025) na Afisa mmoja kutoka wizara ya afya ya jimbo la Darfur Kaskazini ambaye alizungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina.
Afisa huyo amesema idadi ya waliofariki ni pamoja na wale waliofanikiwa kufika hospitalini, na kwamba familia nyingi ziliwazika jamaa zao bila msaada wowote kutokana na hali mbaya ya usalama na ukosefu wa usafiri.
Hayo yanajiri wakati mapigano yamepamba moto eneo la magharibi mwa Sudan kati ya jeshi la taifa na wanamgambo wa RSF wanaouzingira mji huo wa El-Fasher tangu mwaka jana. Mji huo ni eneo la mwisho la mji mkubwa wa Darfur uliopo chini ya udhibiti wa jeshi, na umekuwa ukishambuliwa mara kadhaa na wapiganaji wa RSF.
Maeneo ya migahawa ya kijaami yaliyokuwa yakitoa bure chakula ili kuokoa maisha ya watu, yamefungwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ukosefu wa bidhaa muhimu huku ikiripotiwa kuwa kwa sasa baadhi ya familia huishi kwa kula malisho ya mifugo au mabaki ya chakula kilichotupwa.
