Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa 349, wakiwemo wahalifu sugu 31 ambao kwa muda mrefu walikuwa mafichoni.

Aidha baadhi yao waliwahi kufungwa jela kwa makosa mbalimbali, ikiwemo unyang’anyi wa kutumia silaha (kama mapanga), mauaji, wizi wa kutumia nguvu, pamoja na uvunjaji na uporaji wa pikipiki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Salim Ramadhan Morcase, alitoa taarifa hiyo wakati akizungumzia mafanikio ya operesheni na misako iliyofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

“Mafanikio haya tumeyapata kwa ushirikiano mkubwa na wananchi, kupitia operesheni zilizoanza mwezi Mei hadi Juni mwaka huu, ambapo jumla ya watuhumiwa 349 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali,” alisema Kamanda Morcase.

Aliongeza kuwa kati ya watuhumiwa hao, wahalifu sugu 31 walikuwa wakijificha kwa muda mrefu, na baadhi yao ni wakosaji waliokwisha hukumiwa na kuachiwa kutoka gerezani.

Aidha, Kamanda Morcase alieleza kuwa Jeshi hilo limefanikiwa kuvunja mtandao wa wizi wa runinga (TV), ambapo televisheni nane (8) zimekamatwa ambazo ziliripotiwa kuibwa mkoani Pwani na maeneo ya jirani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea na operesheni hizi, na linawaomba wananchi kuendelea kushirikiana nalo kwa kuwafichua wahalifu walioko katika maeneo yao.