Na Allan Kitwe, JamhuriMedia, Tabora
JESHI la Polisi Mkoani Tabora linawashikiria watu sita kwa tuhuma za kuteka na kuua mwendesha bodaboda Hamis Nchambi (27) msukuma, mkazi wa Kata ya Mbugani katika halmashauri ya manispaa ya Tabora.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, ACP Constantine Mbogambi amethibitisha kukamatwa watuhumiwa hao kutokana na msako mkali uliofanywa na Polisi katika maeneo mbalimbali baada ya kupokea taarifa za mauaji hayo.
Kamanda Mbogambi alieleza kuwa watuhumiwa hao walitumia mbinu ya mmoja wao kujifanya abiria na kukodi pikipiki hiyo siku ya tarehe 13 Januari 2026 majira ya saa 2 usiku ili impeleke nyumbani kwake.
Alifafanua kuwa walipofika eneo la makaburi ya Miemba katika manispaa hiyo ghafla walimteka na kumfunga kamba shingoni, mikononi na miguuni na kisha kumnyonga ili kujipatia kipato kisicho halali.
Mwili wa marehemu ulipatikana kesho yake siku ya tarehe 14 Januari 2026 majira ya saa 9.30 alasiri katika eneo la makaburi hayo, katika Kata ya Miemba, ukiwa umefungwa kamba za manila na mpira shingoni, miguuni na mikononi.
‘Baada ya kupata taarifa tulifanya msako mkali katika maeneo mbalimbali na kufanikiwa kukamata watuhumiwa hao sita na pikipiki aina ya SINORAY yenye na. MC 945 FHY aliyokuwa anaendesha marehemu kabla ya kutekwa’, alisema.
Kamanda Mbogambi aliongeza kuwa katika mahojiano ya awali watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na tukio hilo pamoja na matukio mengine ya utekaji na uporaji pikipiki za abiria katika maeneo mbalimbali.
Alitoa wito kwa waendesha bodaboda na jamii kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo ili kuhakikisha wale wote wanaojihusisha na vitendo visivyokubalika miongoni mwa jamii wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.
Kamanda alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi Mkoani hapa limejipanga vizuri na litaendelea kufanya doria za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ili kukomesha vitendo vya uhalifu na kukamatwa wahalifu wote.





