Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma.
NAIBU Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Omari Kipanga amekabidhi kituo cha huduma kwa wateja cha Wizara hiyo,huku akiwataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa weledi ili kushughulikia changamoto ambazo zipo katika sekta ya elimu.
Kauli hiyo ameitoa leo June 12,2025 jijini hapa wakati akikabidhi kituo hicho ambapo Naibu Waziri huyo amesema kupitia kituo hicho naamini wataweza kushughulikia changamoto mbalimbali ambazo zipo katika Wizara hiyo.
“Kupitia kituo hichi tutaenda kutatua changamoto pamoja na kwenda kufanya kazi kwa weledi lengo letu tunataka wizara yetu izidi kusonga mbele katika masuala ya elimu,”amesema Kipanga.

Kwa upande wake,Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,Prof Caroline Nombo alisema wamekisubiria kituo hicho kwa zaidi ya miaka 2 na wanashukuru kimekamilika na kuanza kutoa huduma.
Amesema walikuwa na Call Centre awali lakini kupitia mradi wa shule bora wamekuwa na contact centre ambayo itawasaidia kujua changamoto mbalimbali.
“Napenda niwahakikishie kituo hicho kitaendea kuboresha Mawasiliano na wadau wake.Tunafahamu sekta ya elimu inamgusa kila mtanzania tunaamini kupitia kituo hichi tutawafikia wengi,”alisema Prof Nombo
Hata hivyo,Katibu Mkuu huyo alisema Wizara itaendelea kukitunza kituo hicho na kuhakikisha huduma zinakuwa bora na kinaendelea kuwepo.



