Na Cresensia Kapinga, JamhutiMedia, Songea.

Jeshi la Polisi Mkoani Ruvuma linawashikilia watu wawili na mwingine wanaendelea kumsaka kwa tuhuma za mauaji likiwemo la mwanamke mmoja kuwauwa watoto watatu kwa kuwachinja shingo na kitu chenye ncha kali wilayani Namtumbo.

Akizungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake leo Julai 25,2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya alilitaja tukio la kwanza kuwa lilitokea Julai 12 mwaka huu Majira ya saa 8, mchana, huko katika Kijiji cha Milonji kilichopo kata ya Lusewa wilayani Namtumbo.

Kamanda Chilya alieleza zaidi kuwa inadaiwa siku ya tukio mtuhumiwa Wende Luchagula (30) mkazi wa kijiji cha Milonji aliwauwa watoto wa mke mwenzake kwa kuwachinja shingo na kitu chenye ncha kali na kwamba chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi.

Kamanda Chilya amewataja watoto waliouwawa kikatili na mama yao wa kambo kuwa ni Lugola Samweli (6),Kulwa Samweli wa umri wa miezi 8 na Doto Samweli mwenye umri wa miezi 8 wote wakazi wa Kijiji cha Milonji.

Alifafanuwa kuwa inadaiwa mume wa mtuhumiwa huyo alikuwa ametoa wake watatu lakini alikuwa anampenda zaidi mke mdogo na watoto wake kitendo ambacho mtuhumiwa hakukipenda nipo akavizia mume wake na mama mzazi wa watoto hao ambaye ni mke mdogo wakiwa wameenda mnadani kisha akaamua kuwauwa kikatili kwa kuwachinja watoto hao shingo na kati yao wawili wakiwa ni mapacha na kwamba miili ya marehemu ilishakabidhiwa kwa familia kwaajiri ya utaratibu wa mazishi na mtuhumiwa alishakamatwa na Polisi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Chilya alilitaja tukio jingine kuwa lilitokea Julai 17 mwaka huu Majira ya saa 2 asubuhi huko katika Kijiji cha Lihale, Kata ya Mkako wilayani Mbinga ambako Adam Mkinga (Chengula) (68) mkazi wa kijiji hicho alikutwa ameuwawa ndani ya zizi la Mbuzi nyumbani kwake kwa kuvunjwa shingo ,kunyongwa na ndugu zake wawili waliotajwa majina kuwa ni Dastan Mkinga mkazi wa Bombambili Songea mjini na Leyson Mkinga mkazi wa Ruhuwiko Songea mjini kisha walikimbia na kutokomea kusikojulikana chanzo kiki ni Imani zakishirikina.

Alisema kuwa baada ya kutokea tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoani humo lilifanya msako mkali wa kuwasaka watuhumiwa hao na ilipofika Julai 24 mwaka huu Majira ya saa 2 asubuhi huko katika eneo la Ruhuwiko Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Mmoja Leyson Mkinga na juhudi za kumtafuta mtuhumiwa wa pili zinaendelea.

Aidha Kamanda Chilya ametoa wito na kuwaasa wana ndoa ambao wanaridhia kuolewa kwenye ndoa ya zaidi ya mke Mmoja kuhakikisha wanakuwa wavumilivu na kutokuwa na wivu wa mapenzi ya kupindukia baina yao na pale inapotokea migogoro yoyoye ndani ya ndoa zao waone umuhimu wa kutumia njia sahihi ya kutatua migogoro hiyo kwa amani.