Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumuufwa mwendesha boda boda Ramadhani Hakimu (19) mkazi wa mateka Manispaa ya Songea ambao inadaiwa kabla ya kumuuwa walimpiga sehemu mbalimbali za mwili kisha wakatokomea kusikojulikana wakiwa na boda boda hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya amesema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 26, mwaka huu, ambapo awali Polisi walipokea taarifa ya tukio hilo la mauaji kupitia kituo kikuu cha Polisi cha Songea, ambapo ilidaiwa kuwa huko katika kata ya Matimira Wilaya ya Songea kuwa Ramadhani Hakimu ambaye ni mwendesha boda boda ameuwawa na watu wasio fahamika kwa kupigwa na kitu Kizito kichwani hadi kusababisha kifo kisha kuondoka na pikipiki yenye usajiri MC 869DXL aina ya Haujoe.

Alisema kuwa baada ya Polisi kupata taarifa hiyo Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji mara moja juu ya tukio hilo na ilipofika Agosti 15, mwaka huu huko katika nyumba ya kulala wageni T-Junction iliyopo Manispaa ya Songea Polisi walifanikiwa kumkamata Damas Atanas (Ngonyani) mkazi wa Kijiji cha Matimira ambaye inadaiwa alishiriki katika tukio la mauaji ya bodaboda huyo.

Alifafanuwa kuwa mtumiwa huyo alipohojiwa kwa kina zaidi na Polisi alikiriki kufanya tukio hilo ambalo alidai kuwa alishirikiana na mwenzake aitwaye Erick Kifaru baada ya kupata taarifa hiyo Polisi iliendelea na msako mkali na Agosti 17, mwaka huu katika Kijiji cha Kiwanga Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Erick akiwa na pikipiki waliyokuwa wameiba akiwa ameibadilisha namba za usajili na kusomeka MC 905 EUJ akifanyia kazi ya boda boda na baada ya kuhojiwa mtuhumiwa alikiri kutenda kosa la mauaji ambaye alidai kuwa walishirikiana na mwenzake ambaye pia alikamatwa na kwamba watuhumiwa wote wawili wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.