Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Wazee wa Mkoa wa Pwani wametoa rai kwa vijana kujitambua, kuishi kwa maadili na kuendeleza uzalendo wa kweli kwa kuitetea nchi yao kupitia njia halali zinazojenga heshima.
Aidha, wamesisitiza wataendelea kuwa sauti ya hekima na utulivu, wakishiriki kutoa ushauri na maoni ya kujenga pale inapohitajika kwa maslahi mapana ya Watanzania.

Kauli hiyo ilitolewa mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Mkoa wa Pwani, John Noah Kirumbi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Disemba 3,2025 kutoa pongezi na kuunga mkono hotuba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa kwa Taifa kupitia mazungumzo yake na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kirumbi alisema ,wazee wa mkoa huo wako tayari kusimama imara na kuwa mstari wa mbele katika kudumisha na kulinda amani, umoja, uadilifu na maadili ya Taifa, ambavyo ni nguzo muhimu za ustawi wa maendeleo.
Alibainisha kuwa ,wanaunga mkono kwa nguvu zote maelekezo, maono na msimamo wa Rais Dkt. Samia yaliyotolewa kupitia hotuba hiyo, ambayo imeonyesha mwelekeo sahihi wa maendeleo ya nchi.
“Rais ameonesha kutambua na kuthamini nafasi ya wazee katika Taifa kama nguzo ya busara na mshikamano. Hilo limetupa faraja na kututia moyo kuendelea kuchangia uongozi wa jamii, na limeimarisha heshima yetu pamoja na kutupa mwanga wa kuendelea kutoa hekima kwa jamii,” alisema Kirumbi.

Hata hivyo, aliongeza kuwa Dkt. Samia ni kiongozi mahiri mwenye maono, hekima na utulivu, ambaye analipa Taifa dira, matumaini na mwelekeo imara wa maendeleo.
Baraza la Wazee mkoani humo limetoa dhamira ya kuendelea kumuunga mkono Rais katika hatua zote anazochukua kwa maslahi ya Taifa, wakiahidi kuendelea kuchangia kwa busara na uzalendo katika maendeleo ya nchi.

