Mamia ya maafisa wa zimamoto wanaendelea kupambana kwa siku ya tatu mfululizo na moto mkubwa wa nyika uliosambaa katika maeneo mbalimbali ya kisiwa cha Chios, nchini Ugiriki, baada ya kutangazwa hali ya dharura.
Juhudi za kuudhibiti moto huo zimehusisha jumla ya wazimamoto 444, wakisaidiwa na ndege nane za kuzima moto, waliotumwa kwenye kisiwa hicho kilichoko kaskazini mashariki mwa bahari ya Aegean.
Moto huo umeteketeza maeneo makubwa ya misitu na mashamba ya kilimo, na kusababisha kuhama kwa mamia ya wakazi kutoka vijiji kadhaa katika siku za karibuni.
Mamlaka za kisiwa hicho zimetangaza tahadhari mpya leo Jumanne, zikiwashauri wakazi wa mji mkuu wa kisiwa hicho, kuondoka kutokana na wingi wa moshi unaotanda kutoka maeneo ya karibu na pwani.
