Na Mwandishi Wetu, Jamhurimedia, Dodoma

WAZIRI wa Kilimo,Mhe.Hussein Bashe amewataka wakulima wa Korosho kusini kuhakikisha shughuli zote zinazohusiana na korosho zinafanyika na kupatikana kusini ili kuondokana na umasikini.

Bashe, amesema hayo jijini Dodoma kabla ya kufungua kikao cha tathmini ya uzalishaji, ubanguaji na masoko ya zao la korosho kwa msimu wa 2024/2025 na kuamua mipango ya msimu wa 2025/2026,kilichohudhuriwa na viongozi wa Bodi ya Korosho,Mamlaka ya usimamizi wa Bandari,Taasisi ya utafiti wa Kilimo, watendaji wa serikali,wabunge kutoka mikoa inayolima korosho,wakulima wa korosho,waenda ghala,wabanguaji na viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa Mikoa na Wilaya.

Amesema watu wengi wanajiuliza kwanini umasikini mkubwa upo kusini licha ya kuwa wazalishaji wakubwa wa korosho huku akifafanua sababu kuwa ni kwa sababu anayesafirisha hatoki kusini ,anayeuza gunia hatoki kusini anayeuza kiutulifu hatoki kusini anayeuza surlfa hatoki kusini anayeendesha ghala hatoki kusini anayeendesha ghala wakala yupo India na Vietnam.

Amesema kuwa tafsiri yake ni kwamba kama korosho imenunuliwa shilingi 3000 inatarajia wachumi waseme gharama za uzalishaji hazitakiwi zizidi asilimia 70 kwahiyo kama asilimia 70 ya 3000 haibaki kusini basi kusini wataendelea kuwa masikini licha ya kuwa wazalishaji wakubwa wa korosho.

“Sasa unawauliza Vyama vikuu vya ushirika Mauzo ya zao la korosho ni Trilioni 2.2 asilimia ngapi ya fedha hii inabaki Kusini,inatakiwa tubadilike Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira mazuri kwa wakulima ndiyo maana hata Juzi tumezindua Benki ya Ushirika ni kwajili ya wakulima ,kakopeni kule mfungue viwanda vyenu.

“Tunataka kuona viutilifu vinatoka Kusini,Gunia zinatoka kusini,Surfer zinatoka kusini ili kumaliza tatizo la umasikini jitihada zenu zinahitajika Rais aliyekuwepo sasa hivi anaupendo anaridhia kumsaidia mkulima kijijini ili aondoke kwenye umasikini,”amesema Waziri Bashe.

Vilevile amewataka wakulima kukubali korosho kuuzwa kwa madaraja kwamba daraja la kwanza za wakulima fulani na gharama ya uuzwaji inakuwa tofauti na daraja lingine.Kama daraja la kwanza itauzwa kwa 5000,walipwe 5000 yao ili yule ambaye atazami korosho yake vizuri asile kwa jasho la mwenzake .

“Imefika wakati hapa tulipo tumefika karibu asilimia 98 ya korosho daraja la kwanza.Tunakampuni ya Manyoni inaitwa RV export inazalisha korosho,inawezekana korosho ya manyoni isifikie ukubwa korosho ya kusini lakini ladha ya korosho ya manyoni ikawa nzuri.

“Hivyo ni lazima muyatofautishe maghala kwamba daraja la kwanza kivyake na daraja la pili kivyake ili watu wapate mapato kutokana na jasho lao,”amesema Bashe.

Hata hivyo Bashe amesema kuwa sasa uzalishaji wa korosho kwa msimu wa 2024/2025 umefikia tani 528,262.23, ongezeko kubwa ikilinganishwa na msimu uliopita. Serikali imeazimia kuongeza uzalishaji huo hadi kufikia tani 700,000 msimu ujao na tani 1,000,000 ifikapo 2030 kama sehemu ya Ajenda ya 10/30.

Pamoja na hayo Waziri Bashe alihimiza umuhimu wa hali ya juu ya ufanisi katika tasnia ya korosho. Alisisitiza kwamba lazima sekta ya korosho ifanye kazi kwa pamoja na kuzingatia malengo makubwa ya serikali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa bodi ya Korosho Tanzania(CBT),Brigedia Jenerali Mstaafu Aloyce Mwanjile(NDC),amesema uzalishaji wa korosho ghafi umeongezeka kutoka tani 310,000 msimu wa 2023/24 hafi kufikia tani 528,000 msimu wa 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 70.

Aidha amesema bei ya korosho ghafi katika minada ya soko la bidhaa (TMS)iliongezeka kutoka shilingi 2190 hadi 4195 kwa kilo moja ya korosho ghafi zenye ubora wa daraja la kwanza.

“Ubanguaji wa korosho unaendelea kuimarika ambapo kiasi cha tani 122,000 zinaendelea kubanguliwa kupitia wabanguaji wakubwa na wadogo waliopo nchini,”amesema Mwanjile.