Na Mwandishi Wetu, Japan

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amenadi vivutio vya utalii vya nchini Tanzania huku akikaribisha wawekezaji kutoka nchini Japan kuwekeza Tanzania.

Waziri Chana amesema hayo leo Mei 26, 2025 katika Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii lililofanyika katika Hoteli ya The Westin jijini Osaka nchini Japan.

“Tanzania ni moja ya nchi ambayo ina utulivu wa kisiasa chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hivyo nawakaribisha kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya utalii”amesisitiza Mhe. Chana.

Aidha, amewahasisha wadau wa utalii nchini Japan kudumisha uhusiano wa Biashara ya utalii kati ya Wakala wa Utalii wa nchini humo na Tanzania na kuitembelea Tanzania ili kukuza na kuendeleza Sekta ya Utalii.

Kongamano hilo lilifunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa aliyeongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki katika Maonesho ya Expo 2025 Kansai Osaka nchini Japan.