Na Mwandishi Wetu

‎WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa zawadi za Heri ya Mwaka Mpya 2026 kwa wazee na watoto kupitia Makao ya Watoto ya Huruma na Makao ya Wazee ya Tushikamane Pamoja Foundation (TPF), yaliyopo Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

‎Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Waziri Dkt. Gwajima alisema kuwa ziara yake katika makao hayo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha ustawi, ulinzi na maendeleo ya watoto, wazee na makundi yote maalum, ambayo yanaendelea kupewa kipaumbele cha juu. Amesema kuwa vituo hivyo vinawakilisha vituo vingine vyote nchini katika zoezi hilo la utoaji wa zawadi.

‎“Napenda kutumia fursa hii kuwaeleza kuwa zawadi hizi za sikukuu za mwisho wa mwaka ninazokabidhi leo, nazitoa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais ana upendo mkubwa kwa watoto na wazee, na anaendelea kuhakikisha ustawi na maendeleo yenu. Zawadi hizi ni ishara ya upendo wake, matumaini na imani aliyonayo kwenu kama Taifa la leo na kesho,” alisema Dkt. Gwajima.

‎Aidha, Waziri Dkt. Gwajima aliwapongeza wadau wa sekta binafsi kwa moyo wao wa kujitolea katika kutoa huduma kwa makundi yenye mahitaji maalum, akisema mchango wao ni muhimu katika maendeleo ya Taifa. Amesisitiza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuhimiza ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za maendeleo; hivyo, Wizara ya Maendeleo ya Jamii imejipanga kuimarisha ushirikiano huo ili kuwafikia walengwa wengi zaidi.

‎Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Nandera Mhando, alisema kuwa Wizara, kwa kushirikiana na Maafisa Ustawi wa Jamii, itaendelea kutembelea na kufuatilia kwa karibu vituo vya makao ya watoto na wazee ili kusikiliza changamoto zao moja kwa moja na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

‎Nao watoto na wazee wa makao hayo wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, kwa upendo na zawadi walizopokea, na wamemtakia Mheshimiwa Rais Heri ya Mwaka Mpya 2026, wakimuombea afya njema, amani na mafanikio katika kuendelea kuliongoza Taifa.