Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, amezindua kliniki ya huduma za msaada wa kisheria (Legal Aid Clinic) mkoani Morogoro, itakayotoa huduma za ushauri na msaada wa kisheria bila malipo kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kusogeza huduma karibu na wananchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kliniki hiyo ya siku mbili, Dkt. Homera amewataka wananchi kuchangamkia huduma hiyo ya kliniki kwani fursa pekee ya kuwahudumia wananchi wenye migogoro mbalimbali ikiwemo ya ndoa, ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, akizungumza na wananchi wa mkoa wa Morogoro (hawapo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa kliniki ya utoaji huduma za msaada wa Kisheria (Legal Aid Clinic) itakayotoa huduma za ushauri na msaada wa kisheria kwa wakazi wa mkoa huo bure, iliyofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani, morogoro. Kulia ni Mhandisi Joseph Masunga Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro.

Huduma zitakazotolewa ni pamoja na uwakili, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), huduma za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), pamoja na utoaji wa elimu ya kisheria.

“Kliniki hii inadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt Rais Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za haki karibu na wananchi na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma,” alisema Dkt. Homera.

Aidha, Waziri Homera alizitaka taasisi na mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na wasaidizi wa kisheria kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa kliniki hiyo, ili kuendelea kuiunga mkono Serikali katika juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa mujibu wa sheria.

Alisema Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuratibu, kusimamia na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria ili kuhakikisha wananchi, hususan wale walioko pembezoni, wanafikia haki kwa wakati.

Bi. Nyangri Bwirle kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), akizungumza na wakazi wa mkoa wa Morogoro waliojitokeza kupata huduma ya vyeti vya kuzaliwa wakati wa hafla ya uzinduzi wa kliniki ya utoaji huduma za msaada wa Kisheria (Legal Aid Clinic), iliyofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani, mkoani humo.

Dkt. Homera aliongeza kuwa awamu ya kwanza ya Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria imepata mafanikio makubwa, ambapo jumla ya wananchi 3,734,157 walifikiwa, wakiwemo wanaume 1,807,440 na wanawake 1,926,717, na kupatiwa elimu kuhusu masuala ya sheria, haki za binadamu, utawala bora pamoja na huduma za msaada wa kisheria.

Katika hatua nyingine, Waziri Homera aliipongeza RITA kwa kazi nzuri wanayoifanya, ikiwemo utoaji wa vyeti vya kuzaliwa na utatuzi wa migogoro ya mirathi na ndoa.

Hata hivyo, alisema bado changamoto ya ukatili wa kijinsia inaendelea kuwepo, hivyo Serikali imejipanga kuimarisha huduma za ushauri wa kisheria na unasihi kwa waathirika na manusura wa ukatili huo, pamoja na kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, aliipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kupitia taasisi zake kwa kuleta huduma hiyo mkoani humo, na kuwataka wakazi wa Morogoro kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Stendi ya Zamani ili kunufaika na huduma hizo bila gharama yoyote.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, (katikati) akikabidhi cheti cha kuzaliwa kwa Bw. Michael Mwenda mkazi wa Morogoro wakati wa hafla ya uzinduzi wa kliniki ya utoaji huduma za msaada wa Kisheria (Legal Aid Clinic), iliyofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani mkoani humo. Kushoto ni Naibu Kabidhi Wasihi Mkuu wa RITA, Bi. Irene Lesulie, Wapili kushoto ni Mhandisi Joseph Masunga Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro. Watatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima na wapili kulia ni Bi. Ester Msambazi, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, kutoka Wizara ya Katiba na Sheria.

“Nawaomba wananchi wa Mkoa wa Morogoro mjitokeze kwa wingi kuchangamkia fursa hii ili kutatua changamoto zenu zinazohitaji msaada wa kisheria,” alisisitiza RC Malima.

RC Malima pia aliomba Wizara kuzingatia ukubwa wa Mkoa wa Morogoro wakati wa utoaji wa huduma hizo, ambapo alipendekeza kliniki za msaada wa kisheria ziwafikie pia wananchi wa maeneo ya mbali, ikiwemo Ifakara, ili kuwapunguzia usumbufu wa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo Morogoro mjini.

Naye Naibu Kabidhi Wasihi Mkuu wa RITA, Bi. Irene Lesulie, alisema cheti cha kuzaliwa ni haki ya msingi kwa kila mwananchi, na kuwasihi wananchi kutumia fursa hiyo kwa kutembelea banda la RITA ili kupata huduma mbalimbali ikiwemo vyeti vya kuzaliwa na masuala ya mirathi.

“Uhitaji wa vyeti vya kuzaliwa ni mkubwa. Kutokana na hali hiyo, RITA kupitia mfumo wa kidijitali wa e-RITA imejipanga kikamilifu kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa,” alisema Bi. Lesulie.

Kwa upande wake, Bi. Faudhia Saidi, mkazi wa Kichangani mkoani Morogoro, alisema amenufaika na huduma za RITA baada ya kupatiwa cheti cha kuzaliwa kwa haraka, na kuwahamasisha wananchi wengine wasio na vyeti hivyo kujitokeza kwa wingi.

“Sikuamini kama ningepatiwa cheti changu cha kuzaliwa ndani ya muda mfupi. Nilidhani ingechukua muda mrefu kukifuatilia,” alisema Bi. Saidi.

Kliniki hiyo ya msaada wa kisheria inashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mawakili wa Serikali, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, ikiwa na lengo la kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili wananchi.

Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Morogoro waliojitokeza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kliniki ya utoaji huduma za msaada wa Kisheria (Legal Aid Clinic), iliyofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani, mkoani humo
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, (katikati) akizungumza na watoa huduma wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), wakati alipotembelea banda hilo wakati wa hafla ya uzinduzi wa kliniki ya utoaji huduma za msaada wa Kisheria (Legal Aid Clinic) itakayotoa huduma za ushauri na msaada wa kisheria kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro bure, iliyofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani, mkoani humo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe Adam Malima, na kulia ni Naibu Kabidhi Wasihi Mkuu kutoka RITA, Bi. Irene Lesulie.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe Adam Malima akiteta jambo na Naibu Kabidhi Wasihi Mkuu wa RITA, Bi. Irene Lesulie, Mara baada ya hafla ya uzinduzi wa kliniki ya utoaji huduma za msaada wa Kisheria (Legal Aid Clinic), kumalizika. iliyofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani, mkoani humo. Kushoto ni Bi. Ester Msambazi, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria, kutoka Wizara ya Katiba na Sheria.