Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam,
Waziri wa Viwanda na Biashara,Dkt.Selemani Jafo kesho anarajiwa kufungua maonesho ya huduma ya kinywa na meno ‘Tanzania Dental Expo’ yatakayofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia kesho kutwa (Ijumaa).
Maonesho hayo ambayo yameandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Tanzania Dental Expo, pamoja na mambo mengine maonesho hayo ya kihistoria yawaleta pamoja wataalamu WA tasnia hiyo kutoka ndani na nje ya Tanzania na maandalizi yamekamilika.
“Kutakuwa na hudima ya vipimo na ushauri bure wa kitaalamu kwa watu wenye matatizo ya afya ya kinywa na meno kutoka kwa wataalamu wabobevu.
Lakini pia, kutakuwa na maonesho ya vifaa tiba vya kisasa vinavyotumika katika kutoa huduma na kuwawezesha watoa huduma wa ndani na nje kubadilishana uzoefu katika kuboresha sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Tanzania Dental Expo Dkt. Ambege Jack Mwakatobe, maonesho hayo yatasaidia kuonyesha pia maendeleo ya tasnia kinywa na MENO hapa nchini, sambamba na kuwaomba wadau mbalimnali na wananchi kujitokeza kwa wingi.
“Tunategemea wataalamu kutoka mabara tofauti ikiwemo bara la Ulaya, Asia na Marekani kuja na teknolojia mbalimbali za kisasa zinazotumika katika kutoa huduma za kisasa za afya ya kinywa na meno,”
“Hivyo, maonesho haya ni fursa kwa wataalamu wetu kutoka hospitali na vituo mbalimbali kupewa mafunzo yanayohusiana na teknolojia ya kisasa inayotumika katika kutoka huduma,” amesema Dkt Mwakatobe.
“Takribani watu bilioni 3.5 duniani wakiwemo Watanzania wana changamoto mbalimbali zinazohusiana na afya ya kinywa na meno,”
“Hivyo, itakuwa ni fursa pekee kwa Watanzania wenye changamoto ya afya ya kinywa na meno kupewa bure huduma ya ushauri na vipimo itakayotolewa wakati wa maonesho hayo na wataalamu waliobobea kwa kutumia vifaa vya kisasa,” amesema Dkt. Mwakatobe ambaye ni mwakilishi wa Tanzania katika shirikisho la Afya ya Kinywa na Meno duniani (FDI).
Naye Mwenyekiti wa bodi ya maonesho hayo Dkt. Baraka Nzobo amesema kuwa maonesho hayo ni muhimu kwa Watanzania na nchi jirani ambapo wataalamu mbalimbali watakusanyika kwa ajili ya sekta hiyo muhimu ya afya ya kinywa ma meno kwa binadamu.
“ Maonesho haya ni fursa kubwa kwa nchi yetu kwani ni kwa mala ya kwanza kufanyika nchini ambapo yataleta wageni wa kimataifa wanaoshughulika na kutoa huduma na matumizi ya vifaa tiba vya kisasa vinavyotumika katika nchi zilizoendelea duniani,” Alisema Dkt. Nzobo
“Kupitia maonesho haya, tunategemea mageuzi makubwa kwa watoa huduma wa sekta ya afya ya kinywa na meno hapa nchini kwa kujifunza teknolojia inayotumika katika kutoa huduma na kuongeza weledi katika kazi zao ,” amesema Dkt. Nzobo.
Aidha Ddkt. Nzobo aliwataka wadau mbalimbali kama Taasisi za kibenki na Bima za Afya kujitokeza kushiriki katika maonesho hayo kwani yataenda kubainisha maeneo mahususi ambayo yatawaweza kuunganisha taasisi hizi na zile za kinywa na meno kuweza kufanya kazi kwa pamoja.
Naye Dkt. Leonora Assevi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi na kushiriki maonesho hayo na kujifunza namna ya kutunza afya zao za kinywa na meno na kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo harufu mbaya ya kinywa, matumizi sahihi ya kupiga mswaki.