Na Mwandishi Wetu, JamhiriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Palamagamba Kabudi, amempongeza mwanazuoni mashuhuri wa Tanzania, Keto Mshigeni, kwa kutunga kitabu kinachoelezea maisha yake, akisema ni hazina muhimu kwa kizazi cha sasa na kijacho kujifunza historia ya safari ya mafanikio kupitia elimu, utafiti na uzalendo.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho jana jijini Dar es Salaam, Waziri Kabudi alisema Profesa Mshigeni ametoa mchango mkubwa si tu katika taaluma ya sayansi ya mimea, bali pia katika kujenga taasisi za elimu ya juu na kuhamasisha vijana wa Kitanzania kuthamini maarifa.

Alisema uamuzi wake wa kuandika kitabu cha maisha yake ni tendo la kishujaa na la kizalendo, kwani linatunza kumbukumbu za historia binafsi yenye mafunzo mapana kwa taifa.

“Wasomi wetu wengi wamefanya makubwa lakini hawajaandika historia zao. Profesa Mshigeni ametuvunja ukimya huo kwa kuamua kusimulia safari yake tangu utotoni, changamoto alizopitia, hadi kufikia mafanikio makubwa kitaaluma na kiuongozi,” alisema Kabudi.

Aidha, alieleza kuwa kitabu hicho kinatoa funzo kuhusu umuhimu wa nidhamu, bidii na uadilifu katika ujenzi wa taaluma na taifa.

Alisema simulizi ya Profesa Mshigeni inaonesha namna elimu ilivyoweza kumbadilisha maisha yake na kumuwezesha kulitumikia taifa kwa viwango vya juu, ndani na nje ya nchi.

Kabudi alisisitiza kuwa Tanzania inahitaji mifano hai ya kuigwa, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linawekeza zaidi katika uchumi wa maarifa.

Aliongeza kuwa hadithi ya Profesa Mshigeni inathibitisha kuwa uwekezaji katika elimu na tafiti ni msingi imara wa maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Profesa Mshigeni alieleza kuwa kuandika kitabu hicho kumetokana na shauku ya kushirikisha uzoefu wake na jamii, ili kuwahamasisha vijana kutokata tamaa wanapokutana na changamoto. Alisema kila mafanikio yana historia ya mapambano, na ni muhimu kizazi kipya kufahamu kuwa mafanikio hayaji kwa urahisi bali kwa juhudi na uthabiti.

Waziri Kabudi alihitimisha kwa kuwataka wasomi wengine, viongozi wastaafu na wataalamu mbalimbali kuandika vitabu vya maisha yao ili kuhifadhi kumbukumbu za taifa na kuchochea mjadala wa kitaaluma.

Alisema hatua hiyo itasaidia kujenga utamaduni wa kujifunza kutokana na uzoefu wa waliotangulia na kuimarisha misingi ya maarifa nchini.