Na Jacob Kasiri, JamhuriMedia, Serengeti
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema serikali itatoa shilingi bilioni 8.1 kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya madaraja na barabara zilizoharibiwa na mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha baadhi ya magari ya watalii kukwama kuendelea na safari kwa muda mrefu. Mvua zilizosababishwa na mabadiliko ya Tabianchi.
Waziri Kijaja alitoa kauli hiyo leo machi 08, 2026 katika Hifadhi ya Taifa Serengeti alipofika kujionea athari za uharibifu wa miundombinu hiyo na kuahidi kuchukua hatua za haraka kukabidhi fedha hizo kwa hifadhi hiyo ili matengenezo hayo yaweze kuanza kwa wakati.
Aidha, Dkt. Kijaji aliongeza, “Niwatake waongoza utalii (tour guides) kufuata maelekezo ya askari wa uokoji waliowekwa na TANAPA katika maeneo yote yaliyokumbwa na athari za mvua hizo. Kwani kuvuka madaraja wakati maji yanapita juu ni kuhatarisha usalama wa dereva, watalii pamoja na chombo unachoendesha.”

Sanjari na hilo pia Dkt. Kijaji alikemea tabia za baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kurusha taarifa za upotoshaji na zisizothibitishwa ya kuwa Hifadhi ya Taifa Serengeti imezuia safari za watalii ndani ya hifadhi hiyo, kwani kufanya hivyo kunalikosesha taifa mapato, makampuni ya utalii pamoja na mtu mmoja mmoja aliyeajiriwa au kujiajiri katika sekta ya utalii.
Naye, Naibu Kamishana wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara – TANAPA Massana Mwishawa alitanabaisha kuwa ujio wa Waziri wa Maliasili na Utalii na kuahidi kutoa fedha hizo kutaondoa changamoto hii na kuifanya miundombinu ya hifadhi kupitika mwaka mzima kuwe na mvua za masika au wakati wa kiangazi.
“Ni matumaini yetu kama taasisi matengenezo ya miundombinu hii iliyoharibiwa itakapokamilika itachagiza ongezeko la watalii na kufikia watalii milioni nane ifikapo june 2030 kama maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassani rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyoelekeza”.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti Ismail Omary alisema kuwa baada athari hizo, hifadhi ilichukua hatua za matengenezo ya dharura ya madaraja na barabara hizo ili ziweze kupitika, kuweka ulinzi na kutoa malazi ya dharura hostel na Rest house kwa wageni na madereva.

“Aidha pia kukwamua magari na wageni waliokwama na tulienda mbali zaidi kuondoa tozo za kukaa zaidi (overstay fees) pale ilipoonekana kuchelewa kwao kumetokana na changamoto ya barabara zilizoharibiwa na mvua hiyo”, aliongeza Kamishna Ismail.
Gharama za fedha hizo bilioni 8.16 zitahusisha ujenzi wa madaraja ya Orangi ya juu, Orangi ya chini, Banagi, Bona, vivuko vya Viboko Naabi, Kalvati katika barabara ya Naabi ha Seronera, pamoja na barabara nyingine zilizoharibiwa na mvua hiyo.












