Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Chalinze

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb), amezindua jengo jipya la Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika Wilaya ya Chalinze.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kikwete amewataka watendaji wa taasisi zote za umma nchini kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wa maeneo husika wanapotekeleza miradi mbalimbali ya Serikali, akisema hatua hiyo itachochea maendeleo.

Aidha, ameipongeza TAKUKURU kwa usimamizi wa fedha za umma na utendaji makini uliowezesha taasisi hiyo kufanikiwa kurejesha zaidi ya sh.bilioni 60.2 kupitia operesheni mbalimbali zilizotekelezwa nchini.

Vilevile, Kikwete ametoa rai kwa watumishi wa TAKUKURU kulilinda na kulitunza na kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi ili kutimiza azma ya Serikali ya kujenga Tanzania isiyo na rushwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema ujenzi wa jengo hilo umegharimu jumla ya sh. milioni 406.49 hadi kukamilika kwake.

Ameeleza kuwa taasisi hiyo ilitenga zaidi ya sh. milioni 414 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo, lakini kutokana na kuzingatia misingi ya maadili, uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, TAKUKURU ilifanikiwa kutumia shilingi milioni 406.49 .