Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti na za pamoja katika kuimarisha mifumo ya chakula ili kuhakikisha ushiriki endelevu wa Tanzania katika ajenda za maendeleo ya kimataifa.

Waziri Kombo aliyasema hayo wakati wa kikao kilichofanyika katika Ubalozi wa Tanzania jijini Addis Ababa, Ethiopia, ambako anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Pili wa Mfumo wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (UNFSS+4), unaofanyika tarehe 27 hadi 29 Julai 2025.

Wakati wa kikao hicho, Waziri Kombo amepokea taarifa kuhusu maandalizi ya mkutano kutoka kwa Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Innocent Shiyo ambaye ameeleza kuwa mkutano huo ni jukwaa la kipekee kwa Tanzania kushiriki katika kujenga ajenda ya kimataifa ya kilimo, kukuza usalama wa chakula, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda, amewasilisha taarifa ya kiufundi akifafanua kuwa mkutano huo unalenga kutathmini utekelezaji wa mageuzi ya mifumo ya chakula kwa misingi ya haki za binadamu, usawa wa kijinsia, utawala bora, na ulinganifu wa sera za kitaifa na kimataifa.

Amesisitiza umuhimu wa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo vijana, wanawake, sekta binafsi, watu wenye ulemavu na mashirika ya kiraia ili kujenga usimamizi shirikishi wa rasilimali za chakula.

Vilevile Balozi Kaganda amebainisha kuwa licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya kilimo nchini, zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, upungufu wa teknolojia ya kisasa, na miundombinu duni ya usambazaji wa chakula, Tanzania imefanikiwa kufikia asilimia 128.3 ya kiwango cha uzalishaji wa chakula, ikionesha kuwa nchi imezalisha chakula zaidi ya mahitaji ya ndani, jambo linaloashiria mafanikio ya juhudi za serikali katika sekta ya kilimo.

Aidha, wajumbe wa kikao wamesisitiza kuwa Tanzania inapaswa kutumia mkutano huo kama fursa ya kujenga ushawishi wa kisera, kuvutia uwekezaji mpya na kuimarisha ushiriki wake katika programu za kikanda na kimataifa.