Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Tanzania imeandika historia mpya katika sekta ya madini baada ya kuanza rasmi kwa ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa ya uchunguzi wa sampuli za madini itakayotoa huduma bora na za haraka kwa wadau wa sekta hiyo ndani na nje ya nchi.
Aidha Maabara hiyo inajengwa katika eneo la Kizota, jijini Dodoma na itagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 14.3.
Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi leo Agosti 25,2025 Jijini hapa,Waziri wa Madini Anthony Mavunde, amesema kuwa ujenzi wa maabara hiyo ni moja ya mafanikio makubwa katika kipindi cha mageuzi ya sekta ya madini yanayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Tunamshukuru Rais Samia kwa dhamira yake thabiti ya kuwekeza katika sekta ya madini,Ujenzi wa maabara hii unakuja miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST), na sasa tunaona Tanzania ikiandika historia mpya ya maendeleo ya kweli,” amesema Mavunde.
Waziri Mavunde ameeleza kuwa kwa muda mrefu bajeti ya sekta ya madini ilikuwa haifanyi vizuri, lakini katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imeongeza bajeti ya sekta hiyo kila mwaka.
Amesisitiza kuwa maabara hiyo si tu itapunguza gharama kwa wachimbaji wadogo, bali pia itaongeza ufanisi katika shughuli za uchimbaji kwa kutoa taarifa sahihi na za kitaalam.
“Kwa sasa tumejielekeza kwenye eneo la utafiti kupitia GST, ambayo ndiyo moyo wa sekta ya madini,tunataka kuwaondoa Watanzania kwenye uchimbaji wa kubahatisha, badala yake tuwape taarifa sahihi za kitaalam zitakazowawezesha kuchimba kwa tija,” ameongeza.

Katika kuhakikisha utafiti unafanyika kwa kina, Waziri Mavunde pia ameeleza kuwa Rais ameridhia mchakato wa ununuzi wa helikopta kwa ajili ya kufanya utafiti wa awali wa kijiolojia, jambo ambalo litaiweka Tanzania kwenye nafasi ya juu katika ramani ya utafiti wa madini barani Afrika.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa GST, Dkt. Notka Huruma Banteze, amesema kuwa maabara hiyo ya kisasa itakuwa na uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina wa sampuli za madini kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu.
Amesema kukamilika kwa maabara hiyo kutawawezesha wadau wa sekta ya madini kupata huduma bora kwa wakati, jambo litakalowezesha maamuzi sahihi na ya haraka kwenye uwekezaji wa madini.
Amesema ujenzi huo unaonesha dhamira ya serikali katika kuwekeza kwenye maeneo ya kimkakati kama utafiti, ambao ndio msingi wa maendeleo endelevu ya sekta ya madini.

Amesema Ujenzi wa maabara hii unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 690, na baada ya kukamilika kwake, Tanzania itakuwa na maabara ya kisasa zaidi ya uchunguzi wa madini katika Afrika Mashariki na Kati.
“Hii ni hatua muhimu inayothibitisha dhamira ya serikali ya kuhakikisha kuwa sekta ya madini inachangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa nchi, kupitia huduma bora, za kisasa na zenye ushindani wa kimataifa, ” amesema.
