Na Mwandishi Wetu, JamburiMeia, Dar
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, anatarajiwa kuzindua kongamano maalum linaloandaliwa na Taasisi ya Umoja wa Watoa Huduma katika sekta ya madini nchini (TAMISA) pamoja na Kamati maalum ya Masoko na Mawasiliano ya taasisi hiyo.
Uzinduzi huo utafanyika kesho tarehe 16 Mei katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, na utahudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya madini kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa TAMISA, Bw. Peter Kumalilwa alisema kuwa uzinduzi huo una lengo la kuimarisha utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa kuitambulisha rasmi mbele ya wadau na mashirika mbalimbali, jambo litakalosaidia kurahisisha utoaji wa huduma katika sekta ya madini.

“Kongamano hili litakuwa jukwaa muhimu la kutoa taarifa kwa wajasiriamali wanaoshiriki au wanaotamani kushiriki katika sekta ya madini, ili waweze kutambua fursa mbalimbali zilizopo na namna ya kunufaika nazo,” alisema Bw. Kumalilwa.
Aliongeza kuwa, pamoja na masuala ya taarifa na elimu, kongamano hilo litajadili kwa kina nafasi ya Watanzania wazawa katika utoaji wa huduma migodini, ikiwa ni pamoja na kuangazia changamoto na fursa zilizopo.
“Kama mnavyofahamu, Mhe. Waziri Mavunde amekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza ushiriki wa wazawa kwenye sekta ya madini,”
“Hivyo, uzinduzi huu ni hatua muhimu kwa wadau wa sekta hii kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” aliongeza Bw. Kumalilwa.
Aidha, alibainisha kuwa zaidi ya Shilingi trilioni 3.1 zimetengwa kwa ajili ya manunuzi ya vifaa na huduma katika migodi mbalimbali, fedha ambazo zinaweza kunufaisha makampuni ya Kitanzania iwapo yatajengewa uwezo na kupewa taarifa sahihi.
“Sisi kama sauti ya wadau wa madini, jukumu letu ni kuhakikisha kwamba watoa huduma wazawa wanapata elimu na taarifa sahihi kuhusu namna ya kushiriki kwenye mnyororo wa thamani wa sekta hii,” alisema.
Ameongeza kuwa TAMISA pia imejipanga kutoa elimu juu ya uanzishwaji wa viwanda vya ndani ili kupunguza utegemezi wa kuagiza bidhaa kutoka nje, na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi hapa nchini.

Bw. Kumalilwa pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira kwa Watanzania kushiriki moja kwa moja kwenye fursa zinazopatikana katika sekta ya madini na kufungua milango ya uwekezaji nchini.
“Mheshimiwa Rais ametupa fursa kubwa kuhudhuria makongamano ya kimataifa ya madini, ambako tumepata fursa ya kujifunza na kuleta ujuzi nyumbani. Pia tunampongeza Waziri Mavunde kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha fursa kwa wazawa,” alisema.
Kwa upande wake, Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa TAMISA, Dkt. Sebastian Ndege, alisema kuwa taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kuwaunganisha watoa huduma wa vifaa na wamiliki wa migodi ili kurahisisha ushirikiano baina yao.
“Mara nyingi wagavi wanakosa njia rasmi za kuifikia migodi. Sisi kama TAMISA tutahakikisha tunawaunganisha ili waweze kufanikisha malengo yao ya kibiashara,” alisema Dkt. Ndege.
Alitoa wito kwa makampuni ya Kitanzania yanayotoa huduma katika sekta ya madini kujiunga na TAMISA ili kunufaika na taarifa, mafunzo na fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia taasisi hiyo.
“Tunawakaribisha wajasiriamali na wagavi wote wa migodini kushiriki katika kongamano hili muhimu, ambalo litakuwa fursa ya kujadili kwa pamoja namna bora ya kuwajengea uwezo Watanzania kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini,” alisema Dkt. Ndege.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa makampuni yanayotoa huduma migodini kutoa kipaumbele kwa Watanzania katika utoaji wa huduma na ajira, ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.