Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga
WADAU wa Kilimo Ikolojia nchini wamemueleza na kumuonesha
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa faida za kilimo ikolojia katika kujenga taifa lenye jamii na mazingira endelevu.
Waziri Mkuu Majaliwa amepata maelezo hayo baada ya kutembelea banda la wadau hao ambao wanashiriki Maonyesho ya Chakula Duniani ya Kitaifa yanayofanyika katika Uwanja wa Mwahako (Usagara) Jijini Tanga.
Akitoa maelezo ya faida ya kilimo ikolojia Mtaalam wa Killimo ikolojia Utafiti na Uchechemuzi kutoka Mtandao wa Baionuai Tanzania (TABIO), Daud Ngosengwa Manongi amesema nguvu ikielekezwa kwenye kilimo hicho jamii na nchi itanufaika kiafya na kiuchumi.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwepo na juhudi madhubuti za uhifadhi na uendelezaji wa nasaba za mimea, uhamasishaji wa uzalishaji wa mazao yasiyopewa kipaumbele, na tafiti shirikishi zinazolenga kuboresha lishe na usalama wa chakula nchini,” amesema.
Wadau hao walieleza kuwa kupitia tafiti hizo shirikishi, matokeo chanya yamepatikana ikiwemo kuidhinishwa kwa aina 13 za mbegu za asili katika Orodha ya Taifa ya Mbegu hatua kubwa katika maendeleo ya kilimo ikolojia nchini.
Manongi alitumia fursa hiyo kufikisha ujumbe wa wadau la kuomba serikali kuwekeza zaidi katika tafiti shirikishi na uhifadhi wa nasaba za mimea ya asili, kwa kuwa tafiti hizo zimeonyesha manufaa makubwa kwa wakulima na jamii kwa ujumla.

Sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Chakula Duniani, wadau wa kilimo ikolojia walishiriki katika mdahalo wa uchechemuzi kuhusu mchango wa mbegu na vyakula vya asili katika kuimarisha uhakika na usalama wa chakula na lishe nchini. Mdahalo huo uliandaliwa kwa ushirikiano wa Shirika la Pelum Tanzania ,FAO, COPRA, na uliwakutanisha taasisi mbalimbali ikiwemo TOSCI, TFNC, Wizara ya Kilimo pamoja na wakulima kutoka mikoa ya Arusha na Tanga.
Katika majadiliano hayo, washiriki walisisitiza umuhimu wa kutekeleza Mkakati wa Kilimo Ikolojia Hai 2023–2030, wakieleza kuwa utekelezaji wake utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo na kuchochea maendeleo endelevu ya kilimo nchini
Ofisa Uchechemuzi kutoka PELUM Tanzania, Pesa Kusaga alisema kupitia maonesho hayo wadau wa kilimo ikolojia walitoa vyeti na zawadi kwa washindi wa mapishi kwenye mazao ya choroko, dengu na mbaazi ambapo kila zao lilitoa washindi watatu.
Kusaga amesema katika shindano hilo mshindi wa kwanza alipata tuzo, cheti, jiko la gesi, seti ya vyombo na fedha shilingi 1,000,000.

Mshindi wa pili alipata tuzo, cheti, jiko la gesi, seti ya vyombo na fedha shilingi 700,000, watatu alipata tuzo, cheti, jiko la gesi, seti ya vyombo na fedha shilingi 500,000 na waanne na kuendelea wamepata cheti na jiko la gesi.
“Shukrani pia ziwafikie wote tulioshirikiana nao, hususan SWISSAID Tanzania, TABIO , TOAM, KIWAMWAKU, JBDI, DDSCDO na wengine wakiwepo wakulima kutoka Arusha, Mwanza, Manyara, Singida, Morogoro na Mtwara,” amesema Kusaga.
