WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Jumanne (Machi 10, 2026) amekagua miundombinu na utendaji kazi wa Bandari ya Kasanga iliyopo Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.
Katika ukaguzi huo, Waziri Mkuu alipata maelezo kuhusu maendeleo ya bandari hiyo ambayo inasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na ni miongoni mwa bandari muhimu katika mwambao wa Ziwa Tanganyika inayohudumia usafirishaji wa mizigo na abiria.
Bandari ya Kasanga ilijengwa kuanzia Aprili 29, 2019 hadi Aprili 28, 2020 kwa gharama ya takribani Sh. bilioni 4.7. Miundombinu iliyopo bandarini hapo ni pamoja na gati la kuegesha vyombo vya majini lenye urefu wa mita 120 na kina cha mita 14, jengo la kusubiria abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria 200 kwa wakati mmoja pamoja na maghala mawili ya kuhifadhi mizigo yenye uwezo wa tani 2,500 kila moja.

Taarifa ya utendaji inaonesha kuwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Desemba 2025, bandari hiyo imehudumia jumla ya tani 3,418 za mizigo, abiria 3,648, meli 11 pamoja na maboti 337. Miongoni mwa mizigo inayohudumiwa katika bandari hiyo ni saruji, makaa ya mawe pamoja na mazao ya chakula kama mahindi, mchele na unga wa sembe.
Aidha, Waziri Mkuu alipata maelezo kuhusu changamoto zinazoikabili bandari hiyo ikiwemo kuongezeka kwa kina cha maji katika Ziwa Tanganyika hali inayosababisha kujaa kwa maji bandarini pamoja na ubovu wa barabara ya kuingia bandarini.
Hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na TPA kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kufanya utafiti wa kitaalamu pamoja na ujenzi wa barabara ya sakafu ngumu yenye urefu wa mita 150 kuelekea bandarini.
Bandari ya Kasanga ni miongoni mwa miundombinu ya kimkakati inayochochea shughuli za usafirishaji na biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa na maeneo jirani.





