WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Rais Mteule na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Biashara ya Afrika (Afreximbank), Dk George Elombi na kuainisha maeneo zaidi ya uwekezaji Tanzania.
Majaliwa amesema anaamini kuwa katika kipindi cha uongozi wa Dk Elombi, benki hiyo itaongeza kwa kiwango kikubwa mchango wake katika kusukuma mbele biashara, maendeleo ya viwanda na uwekezaji wa kimkakati barani Afrika ikiwemo Tanzania.

“Tunapenda kukuhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kujitolea kikamilifu katika ushirikiano wake wa kimkakati na Afreximbank,” amesema.
Katika mazungumzo hayo, Majaliwa amehimiza umuhimu wa Afreximbank kukamilisha mpango wake wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha tiba Tanzania (African Medical Centre of Excellence) ambacho kitakuwa na uwezo wa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na pia kupunguza utegemezi wa rufaa za nje ya nchi kwa matibabu maalum.

Aidha, Waziri Mkuu ameitaka benki hiyo iendelee kuzingatia utekelezaji wa miradi ya kimkakati hapa nchini, akisisitiza kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na miradi yenye tija katika sekta mbalimbali.
“Usaidizi wa kifedha kutoka Afreximbank, utaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemweleza Rais Mteule umuhimu wa kuwekeza katika uchumi wa buluu (blue economy) huku akibainisha kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za baharini ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu.
“Kupitia usaidizi wa Afreximbank, Tanzania inaweza kuendeleza sekta hii kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.”
Kuhusu nishati safi, Waziri Mkuu amemweleza Dk Elombi kwamba Tanzania hivi sasa imeweka msisitizo katika matumizi ya nishati mbadala hivyo itakuwa vema endapo benki hiyo itaunga mkono juhudi hizo ili kuongeza wigo wa matumizi ya nishati hiyo kwa maendeleo endelevu.
