WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba amewaagiza Watendaji Wakuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya tathmini ya miradi yote ambayo malipo ya awali yameshafanyika na hatua za ujenzi zilizofikiwa katika miradi hiyo.
Pia amewaagiza kuangalia kama utekelezaji wa miradi hiyo unaendana na kiwango cha fedha ambacho kimeshatolewa. “Na ikiwa itapatikana miradi ambayo imefanyika chini ya fedha iliyopatikana itakuwa ni hujuma dhidi ya uchumi wa nchi yetu, hawa ni lazima wafike kwenye mkono wa sheria”
Ametoa maagizo hayo leo, Jumatano, Desemba 17, 2025 wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mzani wa. Magari (Mpemba), Mahakama ya Mwanzo Tunduma, soko la Machinga akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Songwe.
“Nimefuatilia, yupo mkandarasi ambaye mlimtoa kule Mbinga, asipate kazi nyingine yeyote hapa nchini, wapatieni wazawa, haiwezekani tumpatie mtu pesa halafu aje atuchezeechezee hapa, wale wote mnaowalipa fedha halafu wanatumia kwenye miradi na madeni yao hawawalipi wazawa wasipate kazi tena”
Amesema kuwa wapo baadhi ya wakandarasi wanaolazimisha fedha za utekelezaji wa miradi inayofanyika nchini Tanzania zilipwe katika benki za nchi zao badala yake katika mikataba itakayoanza kuingiwa waelekezwe kufungua akaunti hapa nchini.
“Haiwezekani mradi unafanyika hapa nchini yeye anataka fedha zilipwe kwenye akaunti za nchi zao, zikifika huko wanalipa madeni, huku miradi inasimama, hapana, kwenye mikataba hakikisheni mnaweka kipengele cha wao kufungua akaunti hapa hapa nchini ili malipo yafanyike hapahapa”
Kadhalika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amewataka viongozi katika maeneo yote nchini kutopuuza changamoto zinazowakabili wananchi na badala yake wafike kwenye maeneo yao na kushirikiana nao katika kuzitatua.
Amesema Serikali ipo kazini na amewahakikishia wananchi kwamba ahadi zote zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi pamoja na yaliyopo katika dira yatatekelezwa kwa vitendo.
Akizungumzia kuhusu usaili wa watumishi wa sekta za afya na elimu, Waziri Mkuu amewataka wahusika wote wa zoezi hilo wazingatie vigezo vilivyowekwa na wasitumie fursa hiyo kuwaweka watu wao. “Msidhulumu watu zingatieni vigezo.”
Pia, Waziri Mkuu amewasihi Watanzania wakiwemo wakazi wa Songwe waendelee kushirikiana kudumisha amani na wakatae kutumika na watu wanaotaka kuivuruga. “Sisi ndio wanufaika wa kwanza wa amani, tuwe na wivu na nchi yetu na haiwezi kuendeshwa kwa rimoti wala vikundi vya wahuni.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi, Godfrey Kasekenya ahakikishe wakati wa utiaji saini mikataba yote ya miradi ya ukandarasi malipo yake yafanyike kupitia benki na ndani ya nchi.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pia amemuagiza Naibu Waziri huyo ahakikishe wakandarasi wanasimamiwa vizuri ili fedha zote wanazolipwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali zitumike katika ujenzi wa miradi husika na si vinginevyo. (mwisho).


