📍Nzuguni, Dodoma

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda, leo ametembelea banda la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.

Mhe. Pinda alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume, Ndg. Raymond Mndolwa, ambaye alieleza kwa kina kuhusu majukumu ya Tume na juhudi zinazoendelea lengo likiwa ni katika kuhakikisha Taifa linakuwa na kilimo cha uhakika kupitia matumizi bora ya miundombinu ya umwagiliaji.

Katika eneo hilo, Mhe. Pinda alitembelea shamba la mfano la Tume lenye miundombinu mbalimbali ya kisasa ya umwagiliaji.

Alielezwa namna miundombinu hiyo inavyoweza kumsaidia mkulima hususani mdogo kupanga kwa ufanisi ratiba ya umwagiliaji kulingana na mahitaji halisi ya mazao, hivyo kuongeza uzalishaji.

Mhe. Pinda alielezea kuridhishwa kwake na kazi inayofanywa na Tume na kuipongeza kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha sekta ya kilimo kupitia mifumo ya kisasa ya umwagiliaji, ambayo inalenga kuongeza tija kwa mkulima na kuimarisha usalama wa chakula nchini.