šAipongeza REA Kwa Kusimamia vyema utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi na Usambazaji umeme Vijijini
šAwasisitiza Watanzania kushiriki Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia
Ataja faida za kutumia Nishati Safi ya Kupikia
Asema Serikali itaendelea kuwezesha wadau wa Nishati Safi ya Kupikia
Atoa wito kwa Sekta Binafsi kushiriki kikamilifu kwenye Kampeni ya Nishati Safi
šKilimanjaro
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ameeleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameipa heshima nchi kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia inayopewa kipaumbele katika mataifa mengi duniani.
Amebainisha hayo Mkoani Kilimanjaro leo Agosti 30, 2025 alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungamo wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya Uzinduzi wa Mpango wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Jeshi la Magereza iliyofanyika katika Gereza la Karanga na kuhusisha taasisi na wadau mbalimbali wa Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema Rais Samia ni kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini na kuwataka wananchi kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati zisizo safi na salama na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Amesema matumizi ya nishati zisizo safi zinamadhara kwa afya ya binaadamu kupitia joto na moshi unaotokana na nishati hizo ambao unatoa kemikali ambayo sio salama kwa afya hivyo kila mmoja abadilike na amhamasishe mwingine katika hilo.
“Rais Samia ametuonyesha njia ni muhimu tukahamasika na kuachana na matumizi ya nishati zisizo salama, tangu tumeanza 2024 takwimu zinaonyesha Jeshi la Magereza lilikuwa likikata mamia ya miti na limekuwa likipata usumbufu kupata kuni za kupikia; kwa kampeni hii misitu yetu inakwenda kusalimika lakini pia afya za wananchi zinanusurika,” amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Alibainisha kuwa hapo awali kabla ya kuanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia, Jeshi la Magereza lilikuwa likitumia zaidi ya tani mia kwa mwaka na sasa baada ya kuanza kutumia Nishati Safi ya Kupikia imewasaidia kupunguza gharama kwa zaidi ya 50%.

“Tunataka ifikapo mwaka 2034; 80% ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia, kwa manufaa yao na vizazi vijavyo,” amesisitiza Mhe. Majaliwa.
Vilevile, Mhe. Kassim Majaliwa ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwezesha na kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kusambaza umeme vijijini na sasa vitongojini.
“REA imefanya kazi kubwa ya kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia lakini pia katika suala la kusambaza umeme, imekamilisha kusambaza umeme vijijini na sasa inasambaza vitongojini, hongereni sana,” amepongeza Mhe. Majaliwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amesema kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza wameendelea kujenga miundombinu ya nishati safi ya kupikia ili kuhamasisha matumizi hayo katika taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Jeremiah Katungu ameishukuru Serikali kwa kuliwezesha Jeshi la Magereza kuweza kutumia nishati safi ya kupikia katika magereza yote nchini na kuipongeza REA kwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Hii yote ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jumhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 zihame kutoka katika matumizi ya nishati chafu na kuhamia katika nishati safi ya kupikia, ” Ameongeza CGP Katungu.



