Waziri Mkuu wa Japan Shigeru Ishiba ametangaza kujiuzulu Jumapili baada ya chini ya mwaka mmoja madarakani. Tangazo lake limekuja baada ya chama chake cha Liberal Democratic Party (LDP), kupoteza wingi wa viti bungeni.
Ishiba, mwenye miaka 68, alisema ataendelea kushika wadhifa huo hadi kiongozi mpya wa chama atakapochaguliwa. Aliongeza kuwa uamuzi wake unalenga kuepusha mgawanyiko zaidi ndani ya chama, akisema: “Sasa ndiyo wakati sahihi wa kujiuzulu.”
Tangazo hilo lilifuatia muda mfupi baada ya Japan kufikia makubaliano ya kibiashara na Marekani, ikipunguza ushuru wa magari kutoka asilimia 25 hadi 15. Ishiba alisema alitaka kwanza kukamilisha mazungumzo hayo kabla ya kuachia madaraka.
Chama tawala cha LDP na mshirika wake Komeito kilipoteza wingi wa viti katika baraza la juu mwezi Julai, baada ya tayari kushindwa kudumisha nafasi yake katika baraza la chini mwaka uliopita. Hali hiyo imesababisha serikali yake kuendesha shughuli kama serikali ya wachache.
Wachambuzi wanasema LDP huenda ikaongeza ushirikiano na chama cha upinzani ili kuunda serikali ya muungano au kuendelea kama serikali ya wachache. Profesa Axel Klein wa Chuo Kikuu cha Duisburg-Essen alisema chama hicho kitahitaji kutoa nafasi zaidi kwa vyama vingine ili kudumisha uthabiti.
Kushindwa kwa LDP, chama kilichotawala karibu bila kupumzika tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kumetokana na hasira za wapiga kura kuhusu kupanda kwa bei na sera za uhamiaji. Vyama vidogo vya mrengo wa kulia, ikiwemo Sanseito chenye misimamo ya kupinga wageni, vilinufaika na hali hiyo.
Katika tathmini ya uchaguzi, LDP pia imelalamika kupoteza wapiga kura wake wa kihafidhina, wengi wakihisi chama kimeelekea kushoto kupita kiasi. Ishiba, anayetambulika kama mwanasiasa wa wastani, alionekana kuwa mbali na msimamo wa mrengo wa kulia ndani ya chama.
Ndani ya LDP sasa kuna mvutano kuhusu mwelekeo wa chama. Baadhi wanataka kurudi kwenye siasa kali za kihafidhina, wengine wakisisitiza msimamo wa kati ili kushirikiana vyema na vyama vingine. Mchanganuzi Klein anatahadharisha hali hii inaweza kutikisa mshikamano wa chama.
Ishiba mwenyewe alisema kujiuzulu kwake ni hatua ya kuzuia mgawanyiko wa kudumu ndani ya chama. Alisisitiza hawezi kuruhusu mvutano wa ndani kudhoofisha uthabiti wa kisiasa wa Japan katika kipindi kigumu.
Wachambuzi wanasema kwamba kujiuzulu kwake kunaacha pengo la uongozi wakati taifa likikabili changamoto za bei, migawanyiko ya kisiasa na ushawishi wa nje, hasa katika eneo la Asia-Pasifiki.
