Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia – Dodoma
Bunge limeidhinisha bajeti ya Sh bilioni 164 kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2025/26, ambapo Waziri Deogratius Ndejembi ameahidi kuibadili sekta hiyo kwa kuweka mifumo madhubuti ya kuondoa migogoro ya ardhi. Vipaumbele saba vimewekwa, ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi.
Waziri Ndejembi amesema Wizara imepokea ushauri wa wabunge na itaongeza matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa e-Ardhi ili kutatua migogoro ya ardhi, hasa ile inayodaiwa kuchochewa na baadhi ya watendaji wa Serikali. Katika mwaka wa fedha huu, Wizara imepanga kushughulikia migogoro 3,000, licha ya kwamba tayari zaidi ya migogoro 5,800 imetatuliwa kiutawala hadi Mei 15, 2025.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, mikakati mbalimbali imewekwa ikiwemo kumilikisha viwanja vilivyopimwa, kusambaza mfumo wa e-Ardhi, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ulipaji wa kodi, pamoja na kuunganisha namba za simu za wamiliki kwa ajili ya kukumbushwa kulipa kodi kwa wakati.
Aidha, Wizara imepanga kubatilisha miliki za viwanja na mashamba yasiyoendelezwa na kuyarejesha katika hazina ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kuwapatia wananchi wenye uhitaji. Ukaguzi wa viwanja na mashamba 1,000 utafanyika ili kubaini wasiotimiza masharti ya umiliki.
Kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP), mipaka ya vijiji 871 imehakikiwa, mipango ya matumizi ya ardhi imeandaliwa kwa vijiji 846, na zaidi ya hati 318,000 za hakimiliki kimila zimesajiliwa. Pia, viwanja zaidi ya 556,000 vimepangwa na kupimwa tangu kuanza kwa Serikali ya Awamu ya Sita.
Kamati ya Bunge imeitaka Serikali kuweka mpango madhubuti kukabiliana na migogoro ya ardhi, hasa uvamizi wa maeneo ya taasisi na mashamba ya Serikali, huku ikishauri fidia kwa wananchi iwe inatolewa kwa wakati na kabla ya uthamini kufanyika.

Wabunge mbalimbali waliishauri Serikali iwachukulie hatua watendaji wanaohusishwa na migogoro, hususan Jiji la Dodoma, huku wakihimiza kuwepo kwa nyumba za bei nafuu zinazomilikiwa na wananchi wengi kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Waziri Ndejembi aliwatoa hofu wabunge kwa kusema Serikali inaendelea kuweka matumizi bora ya ardhi kwa kutumia Sh bilioni 5 kutoka kwa Rais Samia na kuanzisha mfumo wa utambuzi wa uuzaji wa viwanja ili kupunguza malalamiko. Pia, aliagiza Katibu Mkuu kuachana na mifumo ya zamani inayochochea migogoro.
Naibu Waziri Geofrey Pinda alisema Wizara imepunguza idadi ya viwanja vilivyokuwa na migogoro kutoka 3,000 hadi 1,200, na inaunda kamisheni mpya za kushughulikia migogoro hiyo kwa kutumia mifumo iliyoboreshwa. Alitoa wito kwa wabunge kuipitisha bajeti hiyo ili kazi ya utatuzi iendelee kwa kasi zaidi.
