Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma, amewataka Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Jeshi la Polisi kuendelea kuimarisha Amani na usalama kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025 ili uchaguzi huo ufanyike katika hali ya utulivu.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa elimu kwa Mtandao wa Polisi Wanawake pamoja na kuwaaga Askari wakike 27 wanaostaafu kazi kwa mujibu wa sheria Pembe amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuanzisha na kuendeleza Mtandao huo na amehimiza ushirikishwaji wa Askari wa kike katika kazi mbalimbali za Polisi ili kuleta usawa wa kijinsia.

Nae Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Kombo Khamis Kombo, amewataka askari wa kike kuendeleza umoja na mshikamano ili kuimarisha Mtandao huo wa Polisi wanawake ambao umekuwa ukileta tija kwa Jeshi Polisi na Jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi wanawake kwa upande wa Zanzibar, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) PILI FOBBE amesema lengo la kuanzishwa kwa Mtandao wa Polisi wanawake ni kuhamasisha haki na Jinsia ndani ya Jeshi la Polisi.



