Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Waziri wa Afya Janister Mhagama, ametoa wito kwa wanawake kote nchini kuhakikisha wanazingatia usafi wa mwili kwa kutumia bidhaa salama zilizoidhinishwa na mamlaka za udhibiti ili kujikinga na maambukizi hatari na magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, shinikizo la damu, na matatizo ya figo.

Akizungumza leo June 10,2025 jijini Dodoma wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa kwa wanawake na watoto vilivyotolewa na kampuni ya Doweicar Technology Company Ltd, Waziri Mhagama amesema hatua hiyo itaisaidia serikali kuondokana na changamoto kubwa ya gharama za matibabu ya magonjwa hayo ambayo yanazidi kuathiri ustawi wa jamii na kuongeza mzigo kwenye rasilimali za taifa.

“Ongezeko la magonjwa haya linatulazimu kuimarisha mikakati ya kinga, kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu na kuchukua hatua za mapema kulinda afya zao,” amesema Mhagama.

Waziri amewasisitiza wanawake kuwa makini na aina ya bidhaa wanazotumia wakati wa hedhi au baada ya kujifungua na kueleza kuwa matumizi ya bidhaa duni yanaweza kusababisha maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), ambayo ikiwa hayatashughulikiwa kwa wakati huweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya kama matatizo ya figo.

“Napenda kusisitiza kuwa bidhaa kama pedi za SOFTCARE zimeidhinishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), na ni salama kwa matumizi. Tunapaswa kuzielekeza jamii kwenye matumizi ya bidhaa bora kama njia ya kupunguza mzigo wa maradhi yasiyo ya lazima,” amesisitiza Waziri.

Aidha, amewataka wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuendelea kuelimishana kuhusu usafi wa mwili, hususan kwa wanawake na wasichana, ili kusaidia taifa kuwa na kizazi chenye afya bora.

Naye Balozi wa Softcare, msanii maarufu Zari The Boss Lady, aliwahimiza akinamama kutumia bidhaa za kampuni hiyo, akisema zimethibitishwa kuwa salama kwa wanawake na watoto. “Pedi hizi zimetengenezwa kwa pamba halisi, ni rafiki wa mazingira, hazichubui, na zinawafanya wanawake na watoto kuwa huru wakati wote,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amempongeza Softcare kwa msaada huo kwa wanawake wa mkoa wake, na kusema kuwa hatua hiyo inaonyesha dhamira ya kweli ya kampuni hiyo katika kuunga mkono afya ya jamii.

“Tunafurahia kuona bidhaa hizi zimetambuliwa na TBS na kwamba ni salama kwa watumiaji. Ni hatua nzuri kwa afya ya wanawake na watoto wetu,” alisema Senyamule.