…Asema kwa miaka 25 imekuwa kielelezo cha elimu bora
Na Mwandishi Wetu
SHULE za Green Acres zimeanzisha utaratibu wa kusomesha watoto 15 wasiojiweza kila mwaka kama mkakati wa kurejesha faida kwa jamii.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa shule hizo, Jackyline Rushaigo wakati wa hafla ya kutimiza miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule hizo.
Alisema kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu kama wale wenye ulemavu wa ngozi ambao wamekuwa wakiwapokea na kuwasaidia kielimu kwa kuwasomesha bure.

“Tumeona umuhimu wa kusaidia jamii kusomesha watoto hawa na kila mwaka kwenye shule zetu zilizoko mkoa wa Dar es Salaam na Kagera tunachukua wachache tunawasomesha bure,” alisema
Aidha, Jackyline aliipongeza serikali kwa kuanzisha mitaala mipya ya elimu ambayo alisema inawasaidia wanafunzi kusoma zaidi kwa vitendo bafala ya nadharia kama zamani.
“Mitaala hii mipya imeleta hamasa kubwa sana kwa wanafunzi kujifunza kwa vitendo zaidi badala ya kukaa darasani pekee, hii inainua vipaji sana kwani wanasoma kwa vitendo na inamwezesha mwanafunzi kujua anachopenda na kubobea mapema,” alisema
Naye Mkurugenzi wa Elimu ya Msingi Kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Alhaji Abdul Maulid alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia maboresho ya mitaala mipya ya elimu nchini.

Maulid ambaye alimwakilisha Waziri wa Eliumu, Profesa Adolph Mkenda, alisema siku zote Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha elimu inaboreshwa na kutoa wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.
“Ni muhimu kukumbuka kuwa ni kupitia maono ya Rais Samia tumefanikiwa kufanya maboresho ya sera ya elimu ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 sera ina mambo mengi mazuri sana,” alisema
“Kwa miaka 25 shule hii imekuwa bega kwa bega na serikali na imetoa mchango mkubwa sana kwenye sekta ya elimu na naipongeza bpdi na menejimenti ya Green Acres kwa kutimiza miaka 25 ya kutoa elimu bora,” alisema
“Siyo rahisi kuanzisha taasisi kama hii na kwa miaka yote 25 ikasimama kuwa kielelezo bora cha elimu hapa nchini. Tuna shule kama 30,000 tunawatambua na tunawajali sana ndiyo maana tunaendelea kushirikiana,” alisema.

“Nawapongeza sana kwa mafanikio mliyopata kwenye matokeo bora yanayowafanya wahitimu wenu kuvuka mipaka na wengine kufanya kazi kimataifa na mmeweka mazingira bora ya kusomea wanafunzi,” alisema
Aliipongeza shule kwa kuwalea wanafunzi kwenye mazingira ya uadilifu na uzalendo nidhamu na maadili kwa wanafunzi wake.
“Nyote ni mashahidi wa namna gani maadili imekuwa changamoto kubwa lakini nafurahi sana kusikia kwamba mmewekeza sana kwenye masuala ya nidhamu na maadili,” alisema
Pia aliwapongeza kwa kuwekeza kwenye matumizi ya akili mnemba jambo ambalo linakwenda sanjari na mabadiliko ya teknolojia ya karne ya 21.

“Mafanikio yote haya hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa walimu, menejimenti, wazazi na wanafunzi na ndiyo maana wanafunzi wengi waliohitimu Green Acres wana maadili na wanafanya vizuri sehemu zao za kazi,” alisema
Alisema serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika elimu na itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wadau hao ili kuleta ustawi zaidi katika kutoa huduma kwa umma.
“Tunajua kuna changamoto lakini serikali haiwezi kuwaacha, kila litakapotokea jambo tutawaalika tujadiliane namna ya kutatua changamoto,” alisema
Aidha, alisema shule binafsi zikiwemo za dini zimekuwa na mchango mkubwa sana kwenye upatikanaji wa elimu nchini na zimekuwa chachu ya ushindani kwenye maendeleo ya elimu nchini.

“Sekta binafsi kwenye elimu mnatoa mchango mkubwa sana kwenye kodi, ajira na shule binafsi zinaongeza fursa za elimu kwa watanzania na nimefurahi kusikia mbali na wanaolipa mnachukua baadhi ambao hawana uwezo mnawasomesha,” alisema
“kuna yatima, kuna ambao ni maskini na wengine wazazi wao ni wagonjwa wa muda mrefu lakini Green Acres mmewachukua na ndiyo maana mnazidi kuwa juu kitaaluma kwa kutoa elimu bora,” alisema.
