Na Cresensia Kapinga, Songea.
Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limetoa shukrani kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, kwa kuwapatia msaada wa kompyuta sita pamoja na vifaa vingine vyenye thamani ya shilingi milioni 10.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo,kwa niaba ya kamanda wa polisi Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya, mkuu wa kituo kikubwa cha Polisi (OCD)kilichopo manispaa ya Songea, Kilangi Kabisi alisema kuwa vifaa hivyo vitaboresha utendaji kazi wa askari, hususan katika usimamizi wa taarifa, upelelezi, na utunzaji wa kumbukumbu muhimu.
“Tunamshukuru sana Waziri kwa kuona umuhimu wa kutuunga mkono katika kazi zetu. Vifaa hivi vitasaidia kuongeza ufanisi na kasi katika utoaji wa huduma kwa wananchi,” alisema Kamanda huyo.

Kwa upande wake,Katibu wa Mbunge Dk. Ndumbaro, Juma Mpeli alieleza kuwa msaada huo ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha taasisi za umma katika Jimbo la Songea, akisisitiza umuhimu wa teknolojia katika kuboresha utendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Alisema kuwa licha ya kutoa msaada huo pia ameanza ukarabati wa vituo viwili vya polisi ambavyo ni kituo kidogo cha polisi cha Mjimwema na kituo kikubwa cha polisi kilichopo mtaa wa majimaji manispaa ya Songea ambavyo hadi kukamilika vitagharimu kiasi cha sh.milioni 10.

