Na Happy Lazaro, JamhuriMedia, Arusha

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amewataka Maafisa kufanya kazi kwa bidiii na weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa cheo ni dhamana na kinakuja na majukumu.

Dkt.Chana ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akiwavisha cheo manaibu kamishna wawili na kushuhudia uvishwaji vyeo kwa makamishna wasaidizi waandamizi watano waliovishwa vyeo na mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi NCAA Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu).

Dkt Chana amesema kuwa, ni jukumu.lao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na kulinda pamoja na kuhifadhi eneo la Ngorongoro pamoja na kuwa wabunifu na kuongeza mapato ya mamlaka .

Aidha amewataka kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha za mamlaka huku akiwapongeza kwa kupata tuzo hizo kwani inaonyesha kazi inaenda vizuri .

“Nawapongeza sana kwa kupata tuzo hongereni sana na naombeni sana muendelee kuimarisha tuzo hizo kwani mmeipa heshima kubwa mamlaka nimefurahishwa sana na kitendo hicho.”amesema .

Aidha amewataka viongozi wote mliovaa vyeo kuwa chachu ya kufanya kazi kwa kujituma na kuonesha mfano wa kuigwa kwa Maafisa na Askari wanaowaongoza kwani juhudi zao ndizo zitakazochangia kulinda na kuhifadhi eneo la Ngorongoro na kuendelea kuwa kivutio kwa wageni wanaotembelea.

Waliovishwa Cheo na Waziri ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Joas John Makwati aliyepandishwa cheo kuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi, utalii na Maendeleo ya Jamii na Naibu Kamishna wa Uhifadhi Aidan Paul Makalla anayesimamia Huduma za Shirika NCAA.

Kwa upande wa makamishna waliovishwa vyeo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi NCAA Jenerali Venance Mabeyo (mstaafu) ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia idara ya Mipango na uwekezaji, Gasper Stanley Lyimo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Paul Geofrey Shaidi anayesimamia Kitengo cha huduma za Sheria, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Charles Marwa Wangwe anayesimamia Idara ya Uhasibu na fedha.

Wengine ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwin Felician Kashaga anayesimamia Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, na Afisa Uhifadhi Mkuu Daraja la kwanza Mariam Kobelo anayesimamia idara ya Huduma za Utalii na masoko aliyepandishwa cheo kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi.

Kamishna wa Uhifadhi NCAA Abdul-Razak Badru amesema kuwa kwa sasa watumishi wote wa NCAA wameshapatiwa mafunzo ya kijeshi kutoka mfumo wa awali wa kiraia na kuwa mamlaka hiyo itahakikisha inatumia rasilimali ya watumishi waliopo kuongeza nguvu ya kuhifadhi, kulinda, kuendeleza jamii na kuboresha miundombinu ya utalii.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya NCAA Jenerali, Venance Mabeyo (mstaafu) amesema mafanikio ya Ngorongoro yanategemea uadilifu na uwezo wa viongozi wake na kuwaasa viongozi waliovishwa vyeo kubeba matumaini mapya katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.

Mabeyo amempongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Serikali kwa ujumla na wadau wa utalii kwa kuiunga mkono Ngorongoro na hatimae kutangazwa kama Kivutio Bora cha Utalii Barani Afrika kwa mwaka 2025.