Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kisiasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, Mhe. Wang Yi, anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini Tanzania tarehe 9 na 10 Januari 2026, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza na kuimarisha uhusiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili.
Akiwa nchini, Mhe. Wang Yi atapokelewa na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), na pia anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya mazungumzo ya ngazi ya juu yanayolenga masuala ya ushirikiano wa pande mbili na wa kimataifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje, ziara hiyo inalenga kuendeleza uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na China pamoja na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo mpango kazi uliopitishwa wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Beijing, China, Septemba 2024.
Ushirikiano kati ya Tanzania na China umeendelea kuimarika katika sekta za biashara na uwekezaji, ambapo kwa mwaka 2024 thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilifikia takriban dola za Marekani bilioni 5.2. Kampuni za China zimeendelea kuwekeza nchini Tanzania katika sekta za viwanda, kilimo, huduma, usafirishaji, mawasiliano na utalii, zikichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi na ajira.
Kwa mwaka 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ilisajili miradi ya China 343 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1, miradi ambayo ilizalisha ajira zipatazo 82,404, hatua inayoonesha mchango mkubwa wa uwekezaji wa China katika maendeleo ya Tanzania.
Katika sekta ya miundombinu ya uchukuzi, Tanzania na China zimeendelea kushirikiana kwa karibu, ambapo reli ya TAZARA imebaki kuwa alama ya urafiki na ushirikiano wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili. Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860—ikiwemo kilomita 975 upande wa Tanzania na kilomita 885 upande wa Zambia—imeendelea kuwa kielelezo cha mshikamano, umoja na udugu uliodumu kwa miongo kadhaa.
Aidha, ziara ya Mhe. Wang Yi ni uthibitisho wa uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China uliojengwa juu ya misingi ya kuaminiana na kuheshimiana, uhusiano ambao umeendelea kudumu kwa zaidi ya miongo sita tangu kuwekwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, na kuendelea kuwa nguzo muhimu ya diplomasia na maendeleo ya pamoja.


