Na Sabiha Khamis -MAELEZO

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Masoud Ali Mohamed ameitaka Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia Zanzibar (ZPRA) kuwa na ushirikiano katika utendaji kazi ili kutimiza malengo ya Serikaliya kuwaletea wananchi maendeleo.

Ameyasema hayo katika kikao na Bodi ya Wakurugenzi wa ZPRA huko Ofisini kwake Maisara Mkoa wa Mjini Magharibi amesema kuwa endapo Bodi hiyo itaendelea kutoa ushirikiano na Wizara pamoja na Taasisi ya ZPRA katika utendaji kazi itasaidia kufanikisha malengo yaliyoainishwa katika sheria hasa katika utendaji kazi wa ZPRA.

Aidha ameitaka bodi hiyo kufanyakazi iliyoainisha katika sheria ya ZPRA namba 6 ya mwaka 2016 ikiwemo kumshauri Waziri kwa lengo la kuimarisha uchumi na kuongeza ufanisi.

Amefafanua kuwa bodi inajukumu la kumshauri Waziri pamoja na kusimamia utendaji wa taasisi husika ili kuweza kufikia malengo yaliyousudiwa ya kuleta maendelo katika nchi.

Waziri Masoud amesisitiza kuwa na uharaka katika utendaji kazi ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya nane kuweza kupata matokeo ya maendeleo kwa haraka.

“Tunapokuwa na jambo lolote ambalo tunadhani jambo hilo lisingeweza kutekelezeka bila ya kupata ridhaa au ushauri kutoka kwenye bodi, tuweke utaratibu pembeni kwa dhamira njema ili kuharakisha jambo hilo” alieleza.

Akitoa wito kwa wajumbe wa Bodi pamoja na watendaji wa ZPRA amewasisitiza kuwa tayari kusimamia wakiwa wadhibiti ili kupata matokeo chanya ambayo yamekusudiwa yaonekane kwa wananchi, lengo kuzifikisha taasisi za mafuta na gesi katika hatua nyengine za kimaendeleo.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi asilia Zanzibar Dkt. Omar Dadi Shajak amesema mikakati ya kikao ni pamoja na kuweka mbele malengo ya serikali hasa katika masuala ya mafuta na gesi ili kutimiza dhamira ya serikali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji ZPRA Mohamed Slum Said ambae pia Mjumbe wa Bodi hiyo amesema serikali imeazimia kuipeleka Sekta ya mafuta na gesi katika hatua kubwa ya maendeleo na kuimarisha wa nchi.

Kikao hicho kimejadili mipango ya Serikali katika sekta ya mafuta na gesi ili kuwapatia wananchi maendeleo mazuri kupitia sekta hiyo.