Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga ameahidi kuendeleza ushirikiano baina ya serikali na wenye viwanda kuhakikisha anatimiza ndoto za Rais Samia Suluhu Hassan za kuongeza idadi ya viwanda nchini.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wanachama na viongozi wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI), alipowatembelea kwenye ofisi zao jijini Dar es Salaam kujua changamoto zinazowakabili na kuweka mikakati kuzitatua.

Alisema CTI ni wadau wakubwa kwenye maendeleo ya viwanda na ndiyo sababu ameamua kuwatembelea siku za mwanzo baada ya kuingia ofisi akiwa Waziri wa Viwanda.

Alisema ameamua kuanza kutembelea shirikisho hilo kwa kuwa ni muhimu sana kwenye ustawi wa viwanda na linawafikia wadau 18,000 wa sekta hiyo ya viwanda.

Waziri Kapinga alisema maono ya serikali ya awamu ya sita ni kuboresha uchumi wa viwanda kukuza ajira na kuendeleza kustawisha biashara na kukuza viwanda vya ndani.

“Tumezungumza mengi na wenye viwanda na moja kubwa ni kuendelea kushirikiana kama ilivyokuwa ili kutatua changamoto zao na viwanda kuendelea kutoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi,” alisema.

Waziri Kapinga alisema kuelekea mwaka 2030 maono ya serikali ni kuendelea kuboresha uchumi wa viwanda ili kuchochea ongezeko la ajira na ukuaji wa masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Alisema serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuendelea kusimamia sekta ya viwanda ili iendelee kutoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi na utoaji wa ajira.

“Nimefurahi kuja hapa CTI nimezungumza nao mambo mengi na moja ya mambo nimewahakikishia kuendeleza ushirikiano mkubwa ambao upo baina ya serikali na wao wenye viwanda. Wao wenyewe wameniambia kwamba wanashirikiana vizuri na serikali kutatua changamoto zao zinazogusa viwanda,” alisema

“Jukumu langu ni kuuendeleza ushirikiano uliopo ili kukuza sekta hii ya viwanda na yapo mambo mahsusi ambayo wameniambia na nimewapa uhakika kwamba serikali itayafanyia kazi,” alisema Waziri Kapinga.

Aidha, Waziri Kapinga alisema amewaleza wenye viwanda maono ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoahidi kuyafanya ndani ya siku 100 za utawala wake alipokuwa akinadi sera zake kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Mkurugenzi Mkuu wa CTI, Leodegar Tenga alimshukuru Waziri Judith Kapinga kwa kutembelea shirikisho hilo mapematu mara baada ya kuanza kazi.

Alisema ushirikiano mzuri uliopo baina ya serikali na shirikisho hilo umezaa matunda mengi na kuongeza kuwa ni matarajio yake kupitia Waziri Kapinga mengi yatapatikana.

“ Ushirikiano wa CTI na serikali ni mzuri na tunaona mabadiliko yapo, jitihada zipo ila haiwezekani mambo yote yakakamilika kwa muda mfupi, wenye viwanda wanajua hilo cha msingi ni kuwa na subira,” alisema

“Namshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kumteua Waziri Kapinga naamini tutaendelea kushirikiana naye kwa faida ya wenye viwanda na uchumi wa nchi yetu,” alisema Tenga.