Na Mwandishi Wetu, Morogoro
MAELFU Mkoa Morogoroni wavutiwa na mpango wa huduma za msaada wa kisheria bila malipo na kuipongeza serikali wakisema mpango huo siyo tu unasaidia wananchi wenye kipato cha chini tu bali utapunguza migogoro ikiwemo mirathi, ndoa na ardhi.
Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti kwenye Kliniki ya siku mbili ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, zinazotolewabure kupitia taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Wakati wa kliniki hiyo, wananchi haop pia wamefaidika na utoaji wa elimu ya kisheria na huduma za uwakili.
Wkizungumza wakati wa uzinduzi huo, mmoja wa wananchi walionufaika na huduma hizo, Bi. Amina Shabani, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha na kusogeza huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan. Aidha, Bi amina pia aliomba mpango huo uwe endelevu kwa kugusa maisha ya wananchi wengi wanaoshindwa kumudu gharama za kupata huduma za kisheria.
“Tunaishukuru sana Serikali kupitia taasisi mbalimbali ikiwemo RITA kwa kuwa na utaratibu huu unaogusa maisha ya Watanzania wengi, hususan wenye kipato cha chini wanaohitaji msaada wa kisheria,” alisema Bi. Amina.
Aliongeza kuwa ni muhimu kampeni hiyo ikaendelea na kuwafikia wananchi wengi zaidi, wakiwemo wanaoishi vijijini na maeneo ya pembezoni.

Naye Bw. Kombo Muya alisema amevutiwa na zoezi la utoaji wa vyeti vya kuzaliwa linaloendeshwa na RITA, akisema limeondoa usumbufu wa kufuatilia vyeti hivyo hasa kwa wananchi wanaoishi mbali na ofisi za taasisi hiyo.
“Mbali na huduma za vyeti vya kuzaliwa, nimevutiwa pia na huduma za utatuzi wa migogoro ya ndoa, ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia pamoja na utolewaji wa huduma za uwakili. Hizi ni huduma zinazogusa maisha ya Watanzania wengi moja kwa moja, hususan wenye kipato cha chini,” alisema Bw. Muya.
Kwa upande wake, Bi. Faudhia Saidi, mkazi wa Kichangani mkoani Morogoro, alisifu jitihada za Serikali akisema zimesogeza huduma karibu na wananchi.
“Kupitia kliniki hii, nimefanikiwa kupata cheti cha kuzaliwa cha mtoto wangu kwa muda mfupi, jambo ambalo limeniondolea usumbufu wa kukifuatilia katika ofisi ya wilaya,” alisema Bi. Saidi.
Alisifu pia mpango wa utoaji wa elimu ya kisheria kwa wananchi, akisema unasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro katika jamii, hususan ile inayohusiana na masuala ya mirathi, ndoa na talaka.

Naye Bw. Emanuel Semba kutoka Wilaya ya Kilombero alisema kupitia kliniki hiyo amejifunza matumizi ya mfumo wa kidijitali wa e-RITA, uliomwezesha kupata cheti cha kuzaliwa cha mtoto wake kwa kutumia simu yake ya mkononi.
“Kupitia mfumo huu wa e-RITA, nimeweza kupata cheti cha kuzaliwa ndani ya saa 48 za kazi. Hii inaonesha wazi namna Serikali ilivyojipanga kuratibu, kusimamia na kuimarisha mifumo ya huduma za msaada wa kisheria ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati,” alisema Bw. Semba.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mkoa kutoka RITA, Bi. Salima Ruhaka, alisema kupitia kliniki hiyo, maelfu ya wananchi wamefanikiwa kupata huduma mbalimbali, ikiwemo huduma ya vyeti vya kuzaliwa.
“RITA imejipanga kikamilifu kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma mbalimbali ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, kwani ni haki yao ya kisheria,” alisisitiza Bi. Ruhaka.

Aliongeza kuwa kupitia mpango huo uliozinduliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera wa upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa ndani ya masaa 48, RITA imefanikiwa kusajili wananchi 6,864 kwa ajili ya huduma ya vyeti vya kuzaliwa. Kati yao, wananchi 5,462 sawa na asilimia 80 walikidhi vigezo, huku wananchi 1,130 sawa na asilimia 20 hawakukidhi vigezo.
Kliniki hiyo, iliyowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mawakili wa Serikali, Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia, pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi.


