Shirika la mpango wa chakula duniani WFP limetahadharisha kuwa takriban watu milioni 14 wako hatarini kukumbwa na njaa kutokana na kupunguzwa kwa ufadhili.
WFP imesema watu hao wanapatikana katika mataifa ya Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Haiti, Somalia, Sudan na Sudan Kusini wako hatarini kukumbwa na njaa kutokana na kupunguzwa kwa misaada ya kimataifa ya kibinadamu.
Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain amesema shirika hilo linatarajia mwaka huu wa 2025 kupokea chini ya asilimia 40 ya ufadhili ambazo ni sawa na dola bilioni 6,4, kiwango ambacho ni kidogo mno na hakijawahi kushuhudiwa ukilinganisha na bajeti ya mwaka jana iliyofikia dola bilioni 10.
Chini ya utawala wa Rais Donald Trump, Marekani ambayo ndio mfadhili mkuu wa WFP, ilipunguza kwa kiasi kikubwa misaada yake ya kigeni, hatua iliyochukuliwa pia na mataifa mengine na hivyo kuathiri misheni za maendeleo na zile za misaada ya kibinadamu.
