Shirika la Afya duniani, WHO, limesema utoaji chanjo kwa watu walio kwenye hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ebola umeanza jana Jumapili kusini mwa jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mlipuko wa ugonjwa huo hatari uliripotiwa mapema mwezi huu kwenye kitongoji cha Bulape na kusababisha vifo vya watu 16 na wengine 68 wanashukiwa kuwa wameambukizwa.

WHO imesema dozi za awali zipatazo 400 za chanjo aina ya Ervebo zimetolewa na shehena nyingine ya chanjo itapelekwa siku chache zinazokuja.

Miongoni mwa wanaopatiwa chanjo hizo ni maafisa wa afya walio mstari wa mbele na watu inaoaminika huenda watapata maambukizi kutokana na ukaribu wao na waliokwishaambukizwa.