Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
LICHA ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sayansi na teknolojia ya nyuklia duniani, bado kuna mwanya mkubwa wa ushiriki wa wanawake katika sekta hii muhimu.
Changamoto kama mitazamo hasi ya kijamii, idadi ndogo ya wasichana wanaochagua masomo ya sayansi, pamoja na ukosefu wa mifano ya kuigwa, zimeendelea kuwakwamisha wanawake wengi kuingia na kustawi katika fani hii ya kipekee.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Wanawake katika Nyuklia Tanzania (WiNTz), hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam Juni 04, 2025.

Prof. Nombo amesema kuwa WiNTz imeanzishwa kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika nyanja ya nyuklia, sambamba na kusaidia juhudi za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) katika kukuza usawa wa kijinsia katika taaluma za sayansi na teknolojia.
“WiNTz siyo tu Jumuiya bali ni jukwaa la uwezeshaji, ujumuishi na ubora litakalowapa wanawake nafasi ya kushiriki maarifa, kusaidiana na kuleta mabadiliko chanya. Kupitia utetezi, uelekezaji na ushirikiano, wanawake sasa wana nafasi pana ya kuingia na kung’ara katika sekta ya nyuklia,” alisema Prof. Nombo.
Aliongeza kuwa Tanzania, kama nchi inayoendelea, inakabiliwa na changamoto kubwa zaidi katika kuhakikisha wanawake wanajumuishwa kikamilifu katika sayansi ya nyuklia, na hivyo hatua ya kuanzishwa kwa WiNTz inaleta matumaini mapya kwa maendeleo ya kitaifa.
Katika kuonesha dhamira ya dhati ya serikali, Prof. Nombo alieleza kuwa serikali imetenga Shilingi Bilioni Tatu kwa ajili ya kuimarisha masuala ya sayansi nchini, pamoja na kuwasomesha wataalamu wapya. Aidha, alisema kuwa tayari Watanzania sita wamepelekwa nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo ya nyuklia, ambapo wanatarajiwa kurudi na kusaidia mafunzo kwa wengine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) na Rais wa WiNTz, Profesa Najat Mohammed, alisema kuwa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni hatua muhimu katika kuhamasisha wasichana kupenda masomo ya sayansi na kufikia ndoto zao za kuwa wataalam wa nyuklia.
“Sekta ya nyuklia ina fursa nyingi lakini wataalam ni wachache. Tunataka kuwashika mkono wasichana na kuwasaidia kufikia ndoto zao. Jumuiya hii ni njia ya kuhakikisha hawapotei njiani,” alisema Prof. Najat.
Wakati huo huo, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Jangwani, Raula Marya, alieleza kuwa kuanzishwa kwa WiNTz kunampa motisha zaidi kufikia ndoto zake.

Alisema kuwa juhudi zake katika ubunifu zimekuwa zikisukumwa na mazingira ya kupewa nafasi, akitaja mfano wa ubunifu wake wa kifaa cha kuvuta mbu kilichompeleka hadi kwenye maonesho ya wanasayansi nchini Uturuki.
Kwa kuanzishwa kwa WiNTz, Tanzania imejiunga na mataifa mengine yanayojitahidi kuhakikisha kuwa wanawake wanapata nafasi katika sekta ya nyuklia siyo kama watazamaji, bali kama wabunifu, watafiti na viongozi wa mabadiliko.


