Na WAF, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe ameipongeza Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kukamilisha mradi wa upanuzi wa kituo cha upandikizaji figo uliogharimu Shilingi Bilioni 1.5 na kuahidi Wizara ya Afya itahakikisha inaipatia BMH vifaa tiba kwa ajili ya kutolea huduma kwenye kituo hicho.
Dkt. Shekalaghe ametoa ahadi hiyo Agosti 13, 2025 wakati wa ziara yake hospitalini hapo kujionea hali ya utoaji huduma na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Niwapongeze sana BMH kwa kukamilisha mradi wa upanuzi wa kituo cha upandikizaji figo kupitia fedha za mapato ya ndani ya hospitali, Wizara itahakikisha vifaa tiba vinapatikana kwa ajili ya kutoa huduma kwenye kituo hicho,” amesisitiza Dkt. Shekalaghe.
“Huu ni mfano wa kuigwa kwa hospitali kutumia fedha zake za ndani kuwekeza miundombinu kama hii ya kituo cha upandikizaji figo, niombe uongozi wa hospitali kuwasilisha Wizarani maombi ya mahitaji ya bajeti kwa ajili ya vifaa tiba vya kutolea huduma katika kituo hiki,” ameongeza Dkt. Shekalaghe.
Amebainisha kuwa azma ya Serikali ni kuiwezesha miradi ya kutolea huduma kuanza kuhudumia wananchi mara baada ya kukamilika bila kuchelewa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amemwelezea Katibu Mkuu kuwa mahitaji ya bajeti ya vifaa katika kituo hicho ni takriban Shilingi Bilioni 2.3 na kuwa mradi huo ni mpango wa muda mfupi kwa upande wa huduma za matibabu ya figo.
“Kituo hiki cha upandikizaji wa figo ni mpango wa muda mfupi katika kushughulikia magonjwa ya figo lakini tayari hospitali imepata ufadhili kutoka Shirika la TOKUSHIKAI la nchini Japan wa kujenga Kituo cha Umahiri cha Matibabu ya Figo hapa nchini wenye thamani ya Shilingi Bil. 28,” amebainisha Prof. Makubi.
Prof. Makubi ameongeza kuwa, ujenzi wa mradi huo utaanza baadaye mwaka huu na kuwa utakapokamilika pamoja na kutoa utatuzi wa matibabu ya magonjwa ya figo, utasaidia upande wa mafunzo ya kuzalisha Wataalam wa figo na masuala ya utafiti wa magonjwa ya figo hapa nchini na hata nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba wa BMH Dkt. Kessy Shija amesema, BMH ina Wataalam wa kutosha katika huduma ya upandikizaji figo na kwa sasa wameanza matumizi ya teknolojia ya kisasa ya upasuaji wa matundu madogo (Laparascopic Nephrectomy) katika uvunaji wa figo kutoka kwa watu wanaowachangia figo ndugu zao.
Aidha Dkt. Shija amebainisha kuwa moja ya mafanikio muhimu ni kwamba tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo ya upandikizaji figo katika Hospitali ya BMH mwaka 2018 tayari jumla ya watu 52 wameshapandikizwa figo na maendeleo yao ni mazuri.




