Na.Elimu ya Afya kwa Umma

Katika kuhakikisha Elimu ya Afya inayafikia kwa urahisi makundi mbalimbali ya Kijamii hususan kundi la vijana wa kisasa ari maarufu Genz, Wizara ya Afya Afya kupitia Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma imeanzisha Mjadala wa Wazi kupitia mtandao wa Kijamii wa Tiktok wa Elimu ya Afya.

Akizungumzia kuhusu umuhimu wa mjadala huo unaojulikana kwa jina la Tukutane Tiktok Live, Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt.Ona Machangu amesema kupitia mjadala huo utasaidia kwa kasi kubwa vijana kupata taarifa na elimu sahihi kuhusu masuala mbalimbali ya elimu ya Afya kwa vijana wa kizazi cha kidijitali ari maarufu vijana wa Genz na kuepukana na upotoshaji kupitia mitandao.

“Kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia, vijana wengi wamehamia kwenye mitandao ya kijamii, ili kuongeza wigo sasa tumeamua kuwafuata huko na kuanzisha mijadala ya wazi ya elimu ya afya kupitia Tiktok hivyo wanapata wasaa wa kuuliza maswali na kupatiwa ufafanuzi kwani kupitia kipindi hicho tunakuwa na wataalamu mbalimbali wa afya na mada tofautitofauti huwasilishwa”amesema.

Peter Mabwe ni Mratibu wa Mawasiliano ya Afya na Mabadiliko ya Tabia Jamii kutoka Wizara ya Afya,Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma amesema kupitia kipindi cha Tukutane Tiktok Live ni katika kuhakikisha jamii hususan vijana wanakuwa na mabadiliko chanya ya tabia na kufuata misingi na kanuni bora za afya.

Nini mwitikio wa vijana?

Antony Jackson (27) ni Kijana mwenyeji wa Malya Wilayani Kwimba Mkoani Mwanza ambaye kwa sasa anajishughulisha na kazi za kutoza ushuru wa mazao katika manispaa ya Kahama Mkoani Shinyanga amesema siku moja alikuwa anavinjarivinjari (peruziperuzi) katika mtandao wa Tiktok mara akakutana na mubashara(live) ya elimu ya afya na hadi sasa amekuwa mfuatiliaji mzuri.

“Nilikuwa zangu navinjari tiktok,nikakutana na live ya elimu ya afya ,aisee! Nilifuatilia na nilipata madini ya kutosha na siku hiyo walikuwa wanazungumzia wajibu wa mme kumsindikiza mke wake kliniki,hivyo niwasihi tu vijana wenzangu tufuatilie Tiktok Live ya Elimu ya Afya utapata madini ya kutosha”amesema.

Ikumbukwe kuwa Kipindi cha Tiktok Live hufanyika kuanzia saa 2:00 hadi 3:30 usiku na mchokonoa mada katika kipindi hicho ni Grace Msemwa Mtaalamu wa Mawasiliano ya Afya na Mabadiliko ya Tabia Jamii kutoka Wizara ya Afya ambapo mtazamaji na msikilizaji hupata wasaa wa kuuliza maswali kuhusu kitu asichokielewa na kupewa ufafanuzi wa moja kwa moja na wataalamu walioalikwa kutoa mada kwenye kipindi husika.