Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Wizara ya Fedha imeainisha vipaumbele vyake vitano itakavyovitekeleza katika mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa bajeti ya serikali.
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni Kukusanya Mapato kwa Bajeti ya Serikali ambapo Wizara inalenga kukusanya na kusimamia mapato ya jumla ya Shilingi trilioni 50.17 ili kugharamia shughuli za maendeleo na huduma kwa wananchi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Kauli hiyo ameitoa leo Juni 4, 2025, na wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2025/2026 bungeni jijini Dodoma
Akiwasilisha makadirio hayo Waziri huyo ameeleza kuwa kipaumbele kingine ni kulipa kwa wakati deni la serikali linalotarajiwa kuiva, ambalo linakadiriwa kufikia Shilingi trilioni 14.22, huku serikali ikilenga kuhakikisha uhimilivu wa deni hilo.
“Kipaumbe cha Wizara pia ni Kujenga Mfumo wa Pamoja wa Ankara za Malipo
Wizara imepanga kuanzisha mfumo wa pamoja wa kutoa ankara za malipo ya serikali ili kuongeza uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kutoka taasisi mbalimbali za umma, ” amesema.

Ametaja kipaumbele kingine ni kuimarisha Mifumo ya Kielektroniki
Kipaumbele kingine ni kuboresha, kuunganisha na kuimarisha usalama wa mifumo ya kielektroniki inayosimamia fedha na mali za umma ili kudhibiti mianya ya upotevu na kuongeza uwajibikaji.
Kingine ni Kuandaa Sera ya Usimamizi wa Mali za UmmaHatimaye, Wizara itaandaa Sera ya Usimamizi wa Mali za Umma kwa lengo la kuweka misingi imara ya kitaasisi, kisera na kisheria katika uendeshaji na ulinzi wa rasilimali za taifa.
