Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imefanikiwa kuzuia jaribio la kusafirisha kinyume cha sheria madini ya almasi yenye thamani ya dola za Marekani 635,847.66, sawa na takriban shilingi bilioni 1.7, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza.

Tukio hilo lilitokea Mei 18, 2025, ambapo maofisa usalama kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali walifanikiwa kunasa mabegi manne yaliyokuwa yamefichwa almasi zenye uzito wa karati 2,729.82. Almasi hizo zilikuwa mikononi mwa raia mmoja mwenye asili ya India aliyekuwa akijaribu kuzisafirisha kwenda nje ya nchi bila kufuata taratibu za kisheria.

Akitoa taarifa hiyo leo Mei 24, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali jijini Dar es Salaam, alisema tukio hilo ni ushahidi wa uimara wa mifumo ya ulinzi na usimamizi katika sekta ya madini nchini, ikiwa ni sehemu ya mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tunaendelea kusimamia kikamilifu rasilimali za nchi yetu na kuhakikisha hakuna mianya ya wizi au utoroshwaji wa madini. Hili ni tukio la kiashiria kwamba juhudi za serikali zinaendelea kuzaa matunda,” alisema Waziri Mavunde.

Amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu katika sekta ya madini, huku akiwataka wawekezaji na wachimbaji kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alikuwa ameandaa nyaraka za kughushi na hakupata vibali halali kutoka kwa Mamlaka ya Usimamaizi wa Madini  wala vyombo vya serikali vinavyohusika na usafirishaji wa madini.

Waziri Mavunde amepongeza vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na taasisi za serikali kwa ushirikiano uliowezesha kukamatwa kwa almasi hizo kabla ya kufikishwa nje ya mipaka ya Tanzania.