Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza vipaumbele vyake kumi kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 ikiwemo Kuendelea kutangaza utalii ndani na nje ya nchi kupitia,matangazo katika ligi kuu za michezo mashuhuri duniani,
mashindano ya kimataifa, mashirika ya ndege; misafara ya utalii; matamasha ya kimataifa na mitandao mbalimbali ya Kimataifa na Vyombo vya Habari.
Waziri mwenye dhamana hiyo Balozi Dkt.Pindi Chana ameeleza hayo Bungeni leo Mei 19,2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2025/2026. a kuvitaja vipaumbele vingine kuwa ni Kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo maeneo ya malikale pamoja na utalii wa fukwe na mikutano na matukio, meli, michezo, tiba na utamaduni.
Vipaumbe vingine ni Kuboresha miundombinu ya utalii na uhifadhi ikiwemo barabara, viwanja vya ndege na huduma za utalii;Kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa uhifadhi na rasilimali, ufuatiliaji, utangazaji na uendeshaji wa shughuli za utalii na Kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, misitu, nyuki na malikale.
Waziri Chana ameeleza kuwa Wizara hiyo pia imejipanga kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya Misitu na Nyuki, Kuendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa takwimu mbalimbali, kufanya tafiti za kimkakati na kutoa huduma za ushauri zinazohusu masuala ya uhifadhi endelevu wa wanyamapori, misitu na nyuki, malikale na uendelezaji utalii.
“Wizara pia itaendelea kuelimisha na kuhamasisha Jamii kuhusu uhifadhi na
matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, malikale, misitu na ufugaji nyuki;Kuimarisha usimamizi wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za utalii na uhifadhi; na Kuandaa na kufanya Mapitio ya Sera, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali ya kusimamia na kuendeleza Sekta ya Maliasili na Utalii,”amesema.
