Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imewasilisha ombi la bajeti ya shilingi bilioni 340.53 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele vitano vinavyolenga kuimarisha nafasi ya Tanzania katika anga za kimataifa na kuongeza ushiriki wa diplomasia ya kiuchumi.

Akizungumza Bungeni Dodoma Mei 28,2025 , Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 294.998 ni kwa matumizi ya kawaida, huku bilioni 45.540 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

Kuhusu Vipaumbele vya Bajeti ya 2025/2026,Balozi Kombo ametaja maeneo makuu matano yatakayopatiwa kipaumbele ikiwemo Diplomasia ya Uchumi, Kuendeleza uwekezaji, utalii, biashara na upatikanaji wa rasilimali fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Vingine ni Kuimarisha Ushirikiano Kati ya Tanzania na jumuiya/mashirika ya kikanda na kimataifa kwa ajili ya kulinda maslahi ya taifa,Kuongeza Ushawishi wa Tanzania: Katika majukwaa ya kimataifa na masuala mtambuka,Amani na Usalama na Kuwezesha ushiriki wa nchi kwenye juhudi za kudumisha amani kikanda na kimataifa.

“Vipaumbele vingine ni Kuboresha Miundombinu ya Kidiplomasia: Ujenzi na ukarabati wa majengo ya balozi, makazi ya watumishi na vitega uchumi, ” Amesema.

Licha ya hayo ametaja Mafanikio 10 ya Wizara katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, ambapo amesema wizara imefanikiwa kukamilisha na kuzindua Sera ya Mambo ya Nje toleo la 2024,Kusaini mikataba ya ushirikiano na nchi rafiki ikijumuisha rasilimali fedha na ujuzi.

Waziri huyo pia amesema mafanikio mengine ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa kuhusu mazingira, mabadiliko ya tabianchi, nishati safi, na kupambana na uhalifu na kuanzisha Kitengo cha Mikakati na Siasa za Kimataifa (Geo-Political Unit).

Amesema pia Tanzania inaendelea kuongeza ushawishi wake kimataifa, ikiwa ni pamoja na heshima ya Rais Samia kuongeza mchango wa diaspora kwenye maendeleo ya taifa na Kukamilisha tathmini ya Kituo cha Dkt. Salim Ahmed Salim.

“Tumefanikiwa katika Kuboresha utoaji wa taarifa kwa umma kupitia mitandao na njia za kidijitali na kupata kiwanja cha kisasa Kisakasaka, Zanzibar, kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za kisasa za wizara, ” amesema.