Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasili (IUCN) kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wanatarajia kuanzisha Jukwaa la Kitaifa la Biashara za Uchumi wa Buluu litakalolenga kuongeza thamani ya rasilimali za bahari.
Akizungumza leo Agosti 11, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa warsha maalumu iliyoandaliwa na IUCN kwa msaada wa Ubalozi wa Ireland, Mkurugenzi Msaidizi wa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Christian Nzowa, amesema jukwaa hilo litaunda mfumo wa pamoja wa uratibu, kuwezesha ushirikiano wa wadau na kufungua fursa za uwekezaji.

Ameeleza kuwa, warsha hiyo itawezesha kuwekwa msingi wa kuanzishwa kwa jukwaa hilo ambalo linatarajiwa kuanza rasmi baada ya mapendekezo na mpango wa utekelezaji kupitishwa.
“Sekta za uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji zina nafasi kubwa ya kuchochea uchumi wa buluu kutokana na rasilimali zilizopo, ikiwemo ukanda wa Bahari ya Hindi na maziwa makuu matatu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuendeleza dhana ya uchumi wa buluu kupitia Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu iliyozinduliwa Aprili 2024 na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambapo Zanzibar ikiwa imeanzisha Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi pamoja na sera yake tangu 2022,” amesema Nzowa.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana, Nzowa amepongeza Mradi wa Bahari Mali unaoratibiwa na IUCN kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland, ambao umetekelezwa katika maeneo ya Tanga na Pemba.
Amesema kupitia ‘Blue Economy Incubation Initiative’ zaidi ya vikundi 24 vya kijamii vimewezeshwa kuongeza mitaji na kuendeleza biashara zinazolinda mazingira, huku baadhi vikiongeza mitaji yao mara kumi.
“Hadi sasa hekta zaidi ya 90 za mikoko zimeoteshwa na zaidi ya wanachama 400, wakiwemo wanawake na vijana, wamepata mafunzo ya kilimo cha mwani, ufugaji wa majongoo bahari na uvuvi endelevu,” amesema.
Hata hivyo, Nzowa ametaja ukosefu wa jukwaa la pamoja la uratibu kama changamoto kubwa inayokwamisha ushirikiano wa wadau wa sekta hiyo, jambo linalofanya kuanzishwa kwake kuwa kipaumbele cha warsha hiyo.
Ametoa wito kwa sekta binafsi kuwekeza katika miundombinu, teknolojia, masoko na mitaji, na kuwataka vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutumia fursa zitakazopatikana kupitia jukwaa hilo.

Hata hivyo ametangaza mpango wa Wizara kuandaa warsha ya uwekezaji katika uchumi wa buluu katika sekta ya uvuvi, akiuomba ushirikiano wa IUCN na Ubalozi wa Ireland katika utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa IUCN nchini, Charles Oluchina amesema jukwaa hilo wanatarajia litaleta mabadiliko chaya kwa jamii kupitia rasilimali za bahari na kuendeleza fursa za uchumi wa buluu.
“IUCN tumekuwa tukitekelaza mradi wa Bahari Mali eneo la Tanga na Pemba ambalo ni muhimu kwa jeografia ya kiuchumi kwani linabeba utajiri mkubwa wa bainuwaiya bahari, maeneo ya uvuvi na fursa za kibiashara zinazotegemea bahari,” amesema Oluchina.
Ameongeza kuwa, lengo kuu la mradi huo ni kufungua fursa za uchumi wa buluu huku zikihakikisha uhifadhi wa muda mrefu wa haki na shirikishi wa bainuwai na huduma za mifumo ya ikolojia Pwani na baharini.